Saturday 4 July 2009

Chelsea wamsaini Sturridge toka Man City
Chelsea wamemsaini Daniel Sturridge, umri miaka 19, kutoka Manchester City kwa mkataba wa miaka minne.
Sturridge alianza kuchezea Man City Februari 2007 na kufunga mabao manne katika mechi 26 alizocheza na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 24, akiwa ameukataa mkataba mpya hapo Man City, Klabu ya Chelsea itabidi iilipe fidia Man City kwa kumkuza Mchezaji huyo.
Sturridge ni mpwa wa Mchezaji wa zamani wa Derby Dean Sturridge.
Ince arudi tena MK Dons kama Bosi!!
Paul Ince amesaini mkataba wa miaka miwili na Klabu yake ya zamani Milton Keynes Dons kama Meneja na hii ni mara ya pili kwa Ince kuiongoza Klabu hiyo.
Ince anachukua nafasi ya Roberto Di Matteo aliehamia West Bromwich Albion.
Paul Ince anarudi tena MK Dons mwaka mmoja tu baada ya kuihama Klabu hiyo ili kujiunga na Blackburn Rovers ambako hakudumu na alifukuzwa Desemba mwaka jana.
Kwa sasa MK Dons inacheza ligi Daraja la Chini.
Dalglish arudi Liverpool
Kenny Dalglish, ambae alichukua Ubingwa wa England mara 8 katika miaka 14 aliyodumu Liverpool kama Mchezaji na Meneja, amerudi tena Klabuni hapo kama Afisa wa ngazi za Juu kwenye Chuo cha Soka na pia Balozi wa Klabu hiyo.
Akitangaza hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Liverpool, Christian Purslow, amesema: ‘Tunafuraha na hatua hii! ‘
Baada ya kuondoka Liverpool mwaka 1991, Kenny Dalglish akaenda kuwa Meneja huko Blackburn Rovers na kisha Newcastle United na baada ya hapo akawa Mkurugenzi wa Soka huko Celtic Nchini Scotland.
Gibbs aongeza mkataba Arsenal
Beki Chipukizi wa kushoto wa Arsenal, Kieran Gibbs, amesaini kile kinachoitwa ‘mkataba wa muda mrefu’ na Klabu hiyo.
Gibbs, miaka 19, ambae alichukua nafasi ya Beki wa kutumainiwa, Gael Clichy, alipoumia msimu uliopita na kusimama imara kabisa, hivi karibuni ameisaidia Timu ya Vijana ya England ya Chini ya Miaka 21 kuingia Fainali ya Kombe la Ulaya na kufungwa 4-0 na Ujerumani.
Refa Bennett ahamia Kriketi!!
Refa wa Ligi Kuu England Steve Bennett sasa amehamia kwenye mchezo wa Kriketi na atakuwa Mkurugenzi wa Chama cha Waamuzi wa Kriketi ndani ya Bodi ya Kriketi huko England na Wales.
Bennet, miaka 48, ni Refa wa muda mrefu katika Ligi Kuu England na alichezesha Fainali ya Kombe la FA mwaka 2007 na amekuwa Refa wa Ligi Kuu tangu mwaka 1999.
Muhammad Ali kuzuru Old Trafford, Wembley na Uwanja wa Klabu ya Stoke City!!!
Bingwa wa zamani Duniani na Bondia maarufu sana Duniani, Mkongwe Muhammad Ali, atatembelea England hivi karibuni ikiwa ni ziara maalum ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mfuko wa Kituo chake kiitwacho Kituo cha Muhammad Ali.
Akiwa England, Muhammad Ali ataitembelea Old Trafford, nyumbani kwa Mabingwa Manchester United, Uwanja wa Wembley na ule wa Klabu ya Stoke City uitwao Britannia.
Akizungumzia ziara hiyo, Muhammad Ali, amesema: ‘Uingereza iko moyoni mwangu. Nataka kufanya ziara hii si kwa sababu ya kuchangisha pesa tu bali pia kuiona Nchi hiyo nzuri na kuwaona Marafiki zangu na Mashabiki wangu!’

No comments:

Powered By Blogger