Wednesday 1 July 2009

Watano watimuliwa Portsmouth!
Portsmouth imeanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya kwa kuwaondoa Wachezaji watano toka kwenye Kikosi chao.
Wachezaji Noe Pamarot, Lauren, Glen Little, Djimi Traore na Jerome Thomas wamearifiwa kuwa mikataba yao haitaongezwa na wako huru kutimka.
Kati ya hao Beki Djimi Traore ameshapata Klabu Ufaransa kwa kusaini mkataba na AS Monaco huku Mnigeria Kanu bado anatafakari ofa ya nyongeza ya mkataba wa mwaka mmoja aliopewa na Sol Campbell, ambae mkataba wake umekwisha, bado anajadiliana na Portsmouth kuhusu nyogeza.
Beki wa zamani wa Arsenal, Lauren, miaka 32, pamoja na Traore hawakucheza hata mechi moja msimu uliopita na Pamarot alicheza mechi 22.
Mbali ya hao watano waliomwagwa, Glen Johnson, Jermaine Pennant na Armand Traore wameshahamia Klabu nyingine.
Ramsey apewa ofa mpya Arsenal!
Chipukizi Aaron Ramsey, miaka 18, amesaini mkataba mpya na wa muda mrefu Klabuni kwake Arsenal.
Kiungo huyo kutoka Wales aliechukuliwa kutoka Cardiff City kwa Pauni Milioni 5 msimu uliokwisha alichezea mechi 22 Arsenal msimu uliopita.
Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amesema: ‘Alitoa mchango bora. Alionyesha ni Mchezaji mwerevu. Bado ana miaka 18 lakini ataendelea kukua na sisi.’
Wakati huohuo, Arsenal imemtema Kiungo kutoka Ureno, Amaury Bischoff, miaka 22, mwaka mmoja tu tangu atue hapo kutoka Timu ya Ujerumani Werder Bremen.
Bischoff alicheza mechi 4 tu msimu uliopita.
STEVE BRUCE: ‘Kwa Luis Antonio Valencia, Fergie amevua lulu!!’
Mchezaji wa zamani wa Manchester United, Steve Bruce, ambae kwa sasa ni Meneja wa Sunderland na kabla ya hapo alikuwa Klabu ya Wigan, amesema Sir Alex Ferguson amevua lulu kwa kumsaini Luis Antonio Valencia, umri miaka 23, kutoka Wigan.
Valencia amehamia Manchester United jana kwa dau la Pauni Milioni 16 kutoka Wigan ambako Steve Bruce alikuwa Meneja wao kabla ya kuhamia Sunderland msimu uliokwisha ulipomalizika.
Steve Bruce amenena: ‘Antonio ni lulu! Ni Mchezaji mahiri, mchapa kazi kiwanjani na nje ya uwanja ni mwungwana! Ni Winga mwenye nguvu, kasi, akili na ni Mchezaji kitimu! Si haki kumfananisha na Ronaldo lakini yeye ni mpiganaji kupita Ronaldo!’
Steve Bruce amehitimisha kwa kunena ana uhakika Sir Alex Ferguson atafaidika na mchango wa Valencia na kuwa endapo Valencia atajiboresha katika ufungaji basi ni lazima atakuwa Staa mkubwa hapo Old Trafford.
Wakati huohuo, Luis Antonio Valencia ametoa shukrani zake za dhati kwa Klabu ya Wigan kwa kumpa nafasi ya kujiendeleza Ligi Kuu England wakati akiwa bado ni kinda tu. Valencia alianza kucheza Wigan kwa mkopo miaka mitatu iliyopita akitokea Villareal ya Spain.
Valencia amesema: ‘Ni kitu chepesi! Bila ya Wigan nisingekuwa hapa Man U! Wigan ndio imenifikisha hapa! Natoa shukrani zangu kubwa na za dhati kwa Paul Jewell [Meneja aliekuwa Wigan aliposajiliwa], Chris Hutchings na Steve Bruce! Shukran zangu kubwa sana zinaenda kwa Mmiliki na Mwenyekiti wa Wigan, Dave Whelan!’

No comments:

Powered By Blogger