Sunday, 7 February 2010

BIGI MECHI Jumapili Stamford Bridge: Chelsea v Arsenal
Walipofumuliwa na Didier Drogba na Chelsea yake Uwanja wa Emirates mwezi November mwaka jana mabao 3-0, kila mtu aliwafuta Arsenal toka kwenye kinyang’anyiro cha Ubingwa wa Ligi Kuu lakini wenyewe hawakukata tamaa bali walijikongoja na kurudi tena vitani na kufika kileleni huku wakipigana vikumbo na viongozi wenzao Chelsea na Manchester United.
Lakini kipigo cha 3-1 walichokipata Jumapili iliyopita nyumbani kwao Emirates mikononi mwa Manchester United na sasa kuwafanya wawe pointi 7 nyuma ya Man United walio kileleni na pointi 6 nyuma ya Chelsea walio nafasi ya pili, kumeifanya mechi ya Arsenal na Chelsea huko Stamford Bridge leo iwe ya kufa na kupona kwa Arsenal kwani kipigo kingine ni kusema bai bai Ubingwa kwa Arsenal msimu huu.
Hata hivyo, mechi hii na Chelsea ni ngumu mno kwa Arsenal hasa ukichukulia fomu yao ya hivi karibuni na jinsi wanavyopigwa mabao yanayofanana kwa jinsi yanavyofungwa yote yakiwa yanatoka kwenye ‘kaunta ataki’, yaani mashambulizi ya kushtukiza ya wapinzani wa Arsenal.
Juzi, Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, alipasua kuwa kwa vile Arsenal wanamiliki sana mipira ni lazima watakuja mara kwa mara kwenye boksi lako na ukimudu kuwapokonya mpira wakati huo na kufanya shambulizi la kushtukiza na haraka ni lazima utapata bao kwa vile Wachezaji wao karibu wote wanakuwa wamesonga mbele golini kwako.
Na hivyo ndivyo magoli ya Manchester United yalivyopatikana na hata katika mechi ya nyuma yake Arsenal walipocheza na Everton, bao la Everton lilipatikana mara tu kufuatia kona waliyopiga Arsenal golini kwa Everton na Everton kuunasa mpira na kuelekea mkuku golini mwa Arsenal na kufunga bao sekunde kadhaa baada ya kona ya Arsenal.
Kitu cha kutia hofu kwa Arsenal ni kuwa, licha ya Masentahafu wao William Gallas na Thomas Vermaelen kucheza vizuri sana kibinafsi, Timu haichezi kitimu na kwa sasa hawana Mchezaji ambae ni kiongozi wa majeshi uwanjani kama vile alivyokuwepo Tony Adams au Patrick Viera enzi hizo ambae anaweza kuwabatukia wenzake wakikosea au kuwahamasisha
Ndio, Cesc Fabregas ni Mchezaji mzuri sana lakini si kiongozi na hana sifa za uongozi kwani haamrishi wenzake uwanjani.
Ni kitu cha msingi ukipiga kona ni lazima uhakikishe nyuma kwako kuna Wachezaji wa kutosha kuleta ulinzi.
Hili kwa Arsenal halipo.
Ukitaka kubeba mataji lazima uweke uwiano mzuri wa ‘soka tamu’ na misingi ya ulinzi bora.
DONDOO ZA MECHI YA Leo:
Ukweli ni kwamba Arsenal bado hawajaenguliwa kutoka kinyang’anyiro cha Ubingwa wa Ligi Kuu na kwa mechi ya leo kitu kikubwa kwao ni kurudisha heshima yao baada ya kubamizwa mabao 3-1 na Manchester United wiki iliyopita tena wakiwa Uwanja wa nyumbani Emirates.
Vilevile watakuwa na usongo na mechi ya leo wakikumbuka kipigo toka kwa Chelsea cha bao 3-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu.
Lakini msimu uliokwisha, Arsenal waliifunga Chelsea 2-1 hapo hapo Stamford Bridge na hiyo ndiyo mechi ya mwisho kwa Chelsea kufungwa nyumbani sasa zikiwa ni jumla ya mechi 35 bila kufungwa.

No comments:

Powered By Blogger