Mancini apania kuitungua Arsenal nafasi ya 3
Meneja Roberto Mancini wa Manchester City, licha ya kupata kipigo cha 2-1 siku ya Jumamosi kutoka kwa Timu iliyo taabani karibu na mkia Hull City, bado ana imani kuwa Timu yake ina uwezo wa kumaliza ikiwa juu na wanaweza kuwang’oa Arsenal kutoka nafasi ya 3 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Mancini, aliekiri kupandwa hasira na kuwakaripia Wachezaji baada ya kipigo cha Jumamosi, amesema anajiamini kuwa licha ya kuwa pointi 3 nyuma ya Timu ya 4 Liverpool wana uwezo wa kuwapiku Liverpool na kuwang’oa Arsenal nafasi ya 3 kwani wana mechi mbili mkononi na wakishinda hizo watakuwa pointi 2 tu nyuma ya Arsenal.
Leo Man City wanaikwaa Bolton kwenye mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa nyumbani kwao City of Manchester Stadium.
Mancini ametamka: “Nilikasirika baada ya mechi na Hull. Hiyo ni kawaida baada ya mechi kama ile. Naamini tutamaliza Ligi tukiwa juu.”
Meneja huyo Mtaliana amesema Timu za Tottenham, Liverpool, Aston Villa, Manchester City na Arsenal ndizo zinazogombea nafasi za 3 na 4.
Kauli hiyo inamaanisha Ubingwa amewaachia Chelsea au Manchester United.
Mancini, hata hivyo, amekiri Timu yake imeathirika kwa kuwa na majeruhi kama vile Madifenda Joleon Lescott na Kolo Toure.
Pia amebainisha kuwa Timu ina upungufu wa Viungo kwani wana Wachezaji watatu tu kwenye nafasi hiyo nao ni Gareth Barry, Nigel de Jong na Stephen Ireland ambao hawatoshi kwa kucheza msimu mzima.
Wenger awakoromea Waandishi!!
Arsene Wenger amewashambulia vikali Waandishi wa Habari na kudai wanapotosha maneno yake na kuleta picha tofauti na kile anachotamka wakati akihojiwa.
Mara baada ya kipigo cha Jumapili cha Chelsea, ilidaiwa Wenger amesema Arsenal ilikuwa ndio Timu bora na hilo liliwafanya baadhi ya watu, akiwamo Mchezaji wa Chelsea Michael Ballack, kumshambulia Wenger na kudai akifungwa hutoa visingizio kibao.
Wenger alifoka: “Jumapili niliisifia Chelsea. Lakini Waandishi wanachukua neno moja na kuligeuza kuwa stori kubwa. Mlifanya hivyo baada ya mechi na Villa na wamefanya hivyo Jumapili. Mkitaka ntakaa kimya tu! Nimekaa muda mrefu England na najua Timu ikishinda unaweza kusema lolote lakini mimi siku zote nachambua kwa makini na kubainisha nini sawa na nini kosa!”
Wenger aliongeza na kusema bado hawajakata tamaa licha ya kufungwa mfululizo na wapinzani wao wakubwa Manchester United na Chelsea.
Wenger alitamka: “Kitu muhimu ni kushinda tu na baadae tutaona nani Bingwa. Bado kuna mechi 13 na hizo ni pointi 39.”
Wenger vile vile alipuuzia madai kuwa hakutaka kusajili mtu mwezi Januari dirisha la usajili lilipokuwa wazi na alisema walijaribu kusaini Wachezaji lakini haikuwezekana.
Hata hivyo Wenger alikiri Timu yake imeathirika sana kwa kuumia kwa Mastraika wake akiwamo Van Persie.
Alipoulizwa kuhusu kumsajili Mshambuliaji wa Bordeaux Marouane Chamakh, Wenger hakutaka kukubali kama kulikuwa na mazungumzo kati yao ingawa imeripotiwa hivi juzi Chamakh mwenyewe ana lengo la kujiunga na Arsenal.
No comments:
Post a Comment