Friday 12 February 2010

MECHI ZA RAUNDI YA 5 KOMBE LA FA Jumamosi & Jumapili
[saa za bongo]
Jumamosi, Februari 13
[saa 9 mchana]
Chelsea v Cardiff
[saa 9 na nusu mchana]
Southampton v Portsmouth
[saa 12 jioni]
Derby County v Birmingham
Reading v West Bromwich
[saa 2 na robo usiku]
Manchester City v Stoke City
Jumapili, Febryari 14
[saa 10 na nusu jioni]
Bolton v Tottenham
[saa 12 jioni]
Fulham v Notts County
[saa 12 dakika 45]
Crystal Palace v Aston Villa
Chelsea v Cardiff
Chelsea ndio Mabingwa Watetezi wa Kombe hili na wataikaribisha Cardiff huko Stamford Bridge katika mechi ya kwanza kabisa ya Wikiendi mahsusi kwa FA Cup tu.
Chelsea watacheza bila ya Wachezaji wao wawili, Nahodha John Terry aliepewa likizo kupumzisha akili baada ya kuandamwa na kashfa nzito ya kutembea na gelfrendi wa Mchezaji mwenzake Wayne Bridge na Mchezaji mwingine atakaekosekana ni Ashley Cole alievunjika enka.
Southampton v Portsmouth
Klabu iliyo mashakani nje na ndani ya uwanja, Portsmouth, bado inadunda kwenye FA Cup na wanakwaana na jirani zao Southampton inayocheza Daraja la chini.
Portsmouth wako kwenye mtihani mkubwa wa kutaka kufilisiwa na Mamlaka ya Kodi kwa kutolipa Kodi na kesi ipo Mahakamani.
Uwanjani, Portsmouth ndio wanashikilia mkia kwenye Ligi Kuu.
Derby County v Birmingham
Hii pia ni mechi ya Klabu zitokazo maeneo ya pamoja na Birmingham ipo Ligi Kuu na Derby iko Daraja la chini.
Reading v West Bromwich Albion
Reading, walizibwaga Klabu za Ligi Kuu Liverpool na Burnley katika Raundi zilizopita za FA Cup, Raundi hii wanakutana na kigogo wa Daraja la Championship, West Bromwich Albion, ambao wengi wanategemea watarudi Ligi Kuu msimu ujao.
Manchester City v Stoke City
Manchester City v Stoke ni pambano la pili la Raundi hii linalozikutanisha Timu za Ligi Kuu pekee kwenye Raundi hii ya 5 ya FA Cup.
Man City walitolewa kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Carling na Wapwa zao Man United hivyo watakaza uzi ili wasibwagwe nje kwenye Kombe hili pia.
Bolton v Tottenham
Mechi hii ndio ya kwanza katika mechi 3 za Jumapili na ni ya pili inayozikutanisha Timu za Ligi Kuu pekee.
Fulham v Notts County
Notts County waliibwaga Wigan Raundi iliyopita na watataka tena kuibwaga Timu ya Ligi Kuu watakapocheza na Fulham ambayo ina majeruhi kibao.
Crystal Palace v Villa
Crystal Palace ipo kwenye matatizo makubwa kifedha na sasa ipo mikononi mwa Wasimamiza wanaotaka kuifilisi lakini hilo halikuwasimamisha kuibwaga Timu ya Ligi Kuu Raundi iliyopita walipoipiga kumbo Wolves.
Safari hii wapo vitani na Aston Villa Timu ambayo tayari ipo Fainali ya Kombe la Carling na itacheza na Manchester United kwenye Fainali hiyo hapo Februari 28.
Togo yakata rufaa Mahakamani!!
Shirikisho la Soka la Togo limefaili rufaa yao kwenye Mahakama ya Usuluhishi katika Michezo [CAS] huko Uswisi kupinga adhabu waliyopewa na CAF ya kufungiwa kucheza Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mawili yajayo kwa kile kilichoitwa Serikali ya Togo kuingilia masuala ya soka.
Togo walijitoa kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika mwezi uliokwisha huko Angola kufuatia Basi walilokuwa wakisafiria kutoka Congo kuingia Angola Jimbo la Cabinda kushambuliwa kwa risasi na Waasi waliowaua Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa Timu ya Togo.
CAF imedai kuwa Wachezaji wa Togo walikuwa tayari kuendelea na mechi lakini Serikali yao iliwarudisha nyumbani.
Katika Soka Togo kwa sasa inaongozwa na Kamati ya Muda iliyowekwa Januari na FIFA kufuatia mgogoro kwenye Chama cha Soka na Kamati hiyo ndio iliyokata rufaa.

No comments:

Powered By Blogger