Thursday 11 February 2010

Fabregas ang’aka dili ya Barca!!!
Kepteni wa Arsenal Cesc Fabregas amezikataa taarifa kuwa amekubaliana na Barcelona ili ajiunge nao msimu ujao.
Ripoti ambazo chanzo chake ni Spain zimedai kuwa Fabregas amefikia makubaliano kimdomo ili ajiunge na Barcelona ingawa Klabu ya Barcelona haraka imezikana taarifa hizo.
Fabregas amesema: “Wao Barca wamezikataa taarifa hizo, na mimi nazikataa! Mie mawazo yangu yote ni Arsenal tu! Nadhani tunahitaji kuheshimiwa.”
Nae Bosi wa Arsenal, Arsene Wenger, amezitupilia mbali taarifa hizo na kuziita ni upuuzi.
Lakini Baba yake Fabregas amedai mwanawe ataongea na Barcelona mwishoni mwa msimu si kwa sasa kwa vile yupo tu kupigania Ubingwa Arsenal na vile vile amedai ni wajibu wa Klabu hizo mbili kujadiliana mwishoni mwa msimu.
Meneja wa Tottenham atinga kwa Pilato!!!
Harry Redknapp, Meneja wa Tottenham, leo ametinga Mahakamani kujibu mashitaka mawili ya kukwepa kodi aliyoshitakiwa na mwenzake Milan Mandaric ambae ni Mwenyekiti wa Klabu ya Soka Leicester City iliyo Daraja la chini.
Wote wawili wameachiwa nje kwa dhamana hadi Aprili 14 kesi yao itakapoendelea.
Mashitaka haya yanahusu makosa yaliyodaiwa kutendeka wakati Harry Redknapp akiwa Meneja wa Portsmouth na Milan Mandaric akiwa Mwenyekiti wa Klabu hiyo.
Arsenal na Hull City watwangwa faini!!!
Chama cha Soka cha England, FA, kimezipiga faini Klabu za Arsenal na Hull City kwa kosa la kushindwa kuwadhibiti Wachezaji wao kufuatia purukushani iliyotokea Desemba 19 mwaka jana wakati Timu hizo zilipokutana Uwanja wa Emirates.
Vurugu hizo za Wachezaji zilianza kabla ya haftaimu wakati Samir Nasri wa Arsenal alipomtimba Richard Garcia wa Hull City na Stephen Hunt akavutana na Samir Nasri kuhusu tukio hilo na Wachezaji wengine wakajumuika katika shika nikushike hiyo mbele ya Refa Steve Bennett ambae aliwapa Kadi za Njano Nasri na Hunt kwa vurumai hiyo.
Hata hivyo FA ikaamua kuzishitaki Klabu zote mbili na Hull wakakiri kosa lakini Arsenal wakalikataa.
Kamisheni ya Sheria ya FA imeamua Klabu zote zipigwe faini.
Hull City wametakiwa walipe Pauni Elfu 40 na Arsenal Pauni Elfu 20 huku Klabu zote zikipewa onyo la kuchunga mwenendo wao.
Wachezaji Man U wapewa ofu
Sir Alex Ferguson ameipa Timu yake ofu mara baada ya mechi ya Ligi Kuu ya hapo jana waliyocheza na Aston Villa kwa vile wikiendi hii hawana mechi yeyote kwani hii ni wikiendi ya mechi za Kombe la FA na Manchester United wameshatolewa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mechi inayofuata ya Manchester United ni ile ya mtoano wa UEFA CHAMPIONS LEAGUE itakayochezwa huko Milan, Italia dhidi ya AC Milan Jumanne Februari 16.
Ferguson amesema: “Ni matayarisho mazuri kwetu! Wachezaji wapumzike siku chache na Jumamosi watajumuika tena kwa mazoezi ya mechi hiyo ya Ulaya!”
Kiungo Darren Fletcher ameshangilia ofu hiyo na kusema wanastahili hasa baada ya kucheza mechi ya jana na Aston Villa waliyotoka droo ya 1-1 wakiwa mtu 10 kwa zaidi ya dakika 60 baada ya mwenzao Nani kutolewa kwa Kadi Nyekundu.

No comments:

Powered By Blogger