Friday 12 February 2010

Grant matatani na FA!
Meneja wa Timu taabani ndani na nje ya Uwanja, Portsmouth, Avram Grant, ameshtakiwa na Chama cha Soka cha England, FA, baada ya kumvaa Refa Kevin Friend wakati wa mapumziko na kumshambulia kwa maneno Februari 9 huko Fratton Park katika mechi ya Ligi Kuu kati ya Portsmouth na Sunderland iliyokwisha 1-1. Pia, mashitaka hayo yanahusishwa na matamshi yake baada ya mechi.
Grant amepewa mpaka Alhamisi ijayo kutoa utetezi wake.
Grant alikasirishwa na Refa Friend aliewanyima penalti mbili na kumpa Kadi Nyekundu Mchezaji wake Ricardo Rocha na kutoa penalti dhidi yao iliyotoa bao walilofungwa dakika ya 12 ya mchezo.
Refa huyo Friend katika mechi hiyo pia aliwatoa Wachezaji Lee Cattermole na David Meyler wa Sunderland lakini Grant amedai wao ndio walikuwa wakionewa kwa maamuzi yake.
Grant alisema: “Marefa ni wakweli lakini hali ya uwanjani na wao kusoma magazeti kunawatia kasumba! Siwezi kupigana na dunia nzima! Klabu hii imeandamwa kila kona, hatuwezi kusajili, Marefa wanatusakama! Tulipocheza na Man City tulinyimwa penalti na walipata goli la ofasaidi! Na Fulham, ofsaidi ya Zamora! Na Man United, wako mbele 1-0, Evra anashika kwa mikono miwili, hamna penalti! Na Sunderland, penalti mbili! Naweza kupigana na kila kitu lakini saa nyingine huwezi! Pengine ni rahisi kutuonea!”
Refa Mama aweka historia!!
Refa Amy Fearn anawania kuchezesha Ligi Kuu England baada ya kuwa Refa wa kwanza Mwanamke kuchezesha pambano la Ligi Daraja la Championship, ambalo ni chini tu ya Ligi Kuu, alipochezesha dakika 20 za mwisho za mechi ya Ligi kati ya Coventry City na Nottingham Forest waliyoshinda Coventry 1-0 Jumanne iliyopita baada ya Refa Tony Bates kuumia na kulazimika kutoka nje dakika ya 71 ya mchezo.
Mwenyewe Fearn, miaka 31, amesema: “Itakuwa vyema kuchezesha Ligi Kuu lakini najua kupata nafasi ni ushindani mkubwa!”
Fearn alianza kuwa Refa tangu akiwa na miaka 16 na amesema ni matumaini yake kuweka historia hiyo kutakuwa ni changamoto kwa Wanawake wengine kushiriki katika soka.
Fearn alisema: “Uamuzi wa nani anaingia kama Refa wa Akiba hufanywa kabla ya mechi. Refa alietoka, Bates, aliniambia nitulie na nijitahidi tu! Najua Washabiki walivutwa na kuchangamshwa na kuingia kwangu lakini sikumbuki walivyoshangilia! Ilikuwa vyema hamna utata uliotokea dakika zile 20 ingawa Forest walikazana kurudisha bao! Soka inahusu Wachezaji si Marefa!”
Mchezaji alielaumu Refa achunguzwa na FA!!!
Straika wa Bolton Kevin Davies liemponda Refa Mark Clattenburg baada ya kulikataa goli lake safi ambalo lingeipatia ushindi Timu yake ilipocheza na Fulham katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Reebok Stadium na kwisha 0-0 hivi karibuni anachunguzwa na FA kwa matamshi yake.
FA imemwandikia Mchezaji huyo kumtaka ajieleze kuhusu matamshi hayo na maelezo hayo ndio yatatolewa uamuzi ashtakiwe au la.
Davies alidai: “Kila mara akituchezesha, Clattenburg anatuonea! Nilipojua Refa ni nani nilijua hatupati kitu! Siku zote naamini Refa huyo ana chuki binafsi na sisi au mimi!!”
Hata hivyo, Meneja wake wa Bolton Owen Coyle ametetea Mchezaji huyo na kusema alikuwa na haki ya kulalamika na akadai itasikitisha sana ikiwa atashtakiwa kwa kuwa mkweli.

No comments:

Powered By Blogger