Rio afuta rufaa yake!!
Beki wa Manchester United Rio Ferdinand ameiondoa rufaa yake ya kupinga nyongeza ya adhabu ya kufungiwa mechi moja zaidi aliyopewa baada ya rufaa yake ya awali kupinga kufungiwa mechi 3 kwa kosa la kumpiga na mkono Craig Fagan wa Hull City kwenye mechi ya Ligi Kuu kukataliwa.
Ferdinand, ambae amechukua wadhifa wa kuwa Nahodha wa Timu ya Taifa ya England baada ya kutimuliwa John Terry, anatumikia adhabu yake ya kufungiwa mechi 4 na tayari amezikosa mechi mbili zilizopita dhidi ya Portsmouth na Arsenal na pia atakosa mechi mbili zijazo za Aston Villa na Everton.
Ferdinand ataanza tena kucheza kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Carling hapo Februari 28 Man United watakapokutana na Aston Villa.
Hata hivyo adhabu hii haihusu mechi za UEFA na Ferdinand yuko huru kuichezea Timu yake wiki ijayo itakapokutana na AC Milan kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE huko Milan, Italia Februari 16.
Kwa kuifuta rufaa yake hii Ferdinand ameepuka kuongezewa adhabu ya mechi moja zaidi na kuikosa Fainali ya Kombe la Carling endapo rufaa ingeshindwa.
TATHMINI MECHI ZA LIGI KUU LEO:
-Man City v Bolton
Alipoingia Meneja mpya Roberto Mancini Manchester City ilianza kwa wimbi la ushindi lakini hilo limekwisha baada ya kupata vipigo viwili mfululizo kwenye Ligi kutoka kwa Everton na Hull City.
Bolton wako pointi moja tu juu ya Timu tatu za chini.
Timu hizi zilitoka sare 3-3 katika mechi yao ya kwanza ya Ligi lakini wakati huo walikuwa chini ya Mameneja wengine, Mark Hughes kwa City na Gary Megson kwa Bolton, na wote wamefukuzwa.
-Portsmouth v Sunderland
Portsmouth ndio wako mkiani Ligi Kuu na wanakabiliwa na matatizo makubwa nje ya uwanja yakiwemo kubadilika kwa Wamilikaji wa Klabu na ya kifedha.
Mechi yao ya mwisho walikung’utwa bao 5-0 na Manchester United.
Lakini Sunderland nao wako kwenye kipindi kigumu cha kutoshinda mechi 11 sasa na pia watakumbuka wiki mbili zilizokwisha uwanja huo huo wa Fratton Park walifungwa na Portsmouth na kubwagwa nje ya Kombe la FA.
-Fulham v Burnley
Chini ya Meneja mpya Brian Laws ambae alikuwa hajashinda katika mechi 4, Burnley walipata ushindi wao wa kwanza Jumamosi walipoifunga West Ham nyumbani. Lakini Burnley ugenini ni wabovu na wanakutana na Fulham ambao nyumbani ni jiwe gumu.
-Wigan v Stoke City
Stoke City huwa si wazuri mechi za ugenini na wamefunga bao 4 tu katika mechi 11 za ugenini.
Timu hizi zilitoka sare 2-2 katika mechi yao ya kwanza hapo mwezi Desemba huku Mchezaji wa Wigan Maynor Figueroa akifunga bao ambalo pengine ni la msimu kwani aliupiga mpira akiwa nusu ya kwao ya uwanja.
No comments:
Post a Comment