Saturday, 29 May 2010

Eto’o atishia kujitoa Kombe la Dunia!!!
Samuel Eto'o amedokeza huenda akajitoa kwenye Kikosi cha Cameroun cha Kombe la Dunia kufuatia lawama alizobebeshwa na Mkongwe Roger Milla.
Roger Milla, alieng’ara Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 1990 huko Italia, amedai Eto’o hajitumi ipasavywo anavyochezea Nchi yake kama anavyojitutumua alipokuwa FC Barcelona na sasa Inter Milan.
Milla alikaririwa akisema: “Amefanya mengi kwa Barcelona na Inter Milan lakini hajafanya lolote kwa Cameroun!”
Eto'o ndie anaeonekana nyota na mkombozi wa Cameroun na ndie anaeongoza katika historia ya Cameroun kwa kuwa Mfungaji Bora akiwa na Mabao 44 katika Mechi 94 za Nchi yake.
Kauli ya Milla imemchukiza Samuel Eto’o na mwenyewe amedai analalamikiwa bila sababu na Watu wenye uchungu usio na msingi.
Eto’o, ambae wikiendi iliyokwisha aliisaidia Klabu yake Inter Milan kutwaa Klabu Bingwa Ulaya walipoifunga Bayern Munich 2-0, amehoji: “Hivi kuna faida yeyote mie kwenda Kombe la Dunia?”
Eto’o akaongeza: “Nina siku kadhaa za kutafakari kama kuna umuhimu mimi kucheza Fainali hizo. Siku zote kabla Mashindano makubwa wanaibuka Watu wenye kinyongo!”
Huku akionekana mwenye uchungu alipohojiwa na Kituo cha TV Canal Plus, Eto’o alisema: “Yeye Milla kaifanyia nini Cameroun? Hajashinda Kombe la Dunia! Alifika tu Robo Fainali na Kikosi kizuri! Si kwa sababu waliweka historia kwa kucheza Kombe la Dunia wakiwa na Miaka 40 ndio waanze kusema Watu!”
Mwishowe, Eto’o akahoji: “Unashangaa, unajiuliza: hivi hawa ni Watu wangu? Ni kweli Watu wangu? Kuna faida kwenda Kombe la Dunia?”
Real kumtangaza ‘El Especial’ J’Tatu
Jumatatu Real Madrid itamsimika Jose Mourinho kama Kocha wao mpya kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini aliefukuzwa Jumatano iliyopita na hatua hii inafuatia makubaliano yaliyofikiwa jana kati ya Marais wa Klabu za Inter Milan na Real Madrid, Massimo Moratti wa Inter Milan na Florentino Perez wa Real, ya jinsi Inter itakavyolipwa fidia kwa Mourinho kuukatisha Mkataba wake unaotakiwa kwisha 2012.
Katiba Mkataba huo wa Mourinho, anaesifika kama The Special One’ na sasa anaitwa ‘El Especial’ huko Spain ikimaanisha ‘Mtu Spesheli’, na Inter kuna kipengele kinachotaka Inter ilipwe Pauni Milioni 13.5 ikiwa Mkataba utakatishwa.
Mourinho alijiunga na Inter Septemba 2008 na Jumamosi iliyokwisha aliiwezesha Inter kuchukua UEFA CHAMPIONS LIGI pamoja na Makombe ya Coppa Italia na Serie A na hivyo kuweka historia ya kuwa Klabu ya kwanza Italia kushinda Trebo [Vikombe vitatu].
MECHI YA KIMATAIFA YA KIRAFIKI:
Republic of Ireland 3 Algeria 0
Algeria ambao wako Fainali za Kombe la Dunia jana huko Dublin walipigwa bao 3-0 na Republic of Ireland Uwanjani Croke Park.
Mabao ya Ireland yalifungwa na Paul Green dakika ya 31 na mbili kupitia Nahodha wao Robbie Keane, dakika ya 52 na 85, kwa penalti.
Ireland walikosa kucheza Fainali za Kombe la Dunia walipotolewa na Ufaransa kwa bao la utata mkubwa wakati Thierry Henry alipokontroli mpira kwa mkono na kumpasia William Gallas aliefunga bao la kusawazisha na hivyo kuifanya Ufaransa ifuzu.
LEO MECHI ZA KIRAFIKI ZA MATAIFA:
Jumamosi, 29 Mei 2010
[saa za bongo]
Azerbaijan v FYR Macedonia, [saa 12 jioni]
Congo DR v North Korea
Hungary v Germany, [saa 3 usiku]
Iceland v Andorra, [saa 4 usiku]
New Zealand v Serbia, [saa 12 na robo usiku]
Norway v Montenegro, [saa 11 jioni]
Poland v Finland, [saa 12 jioni]
Slovakia v Cameroon, [saa 9 mchana]
Spain v Saudi Arabia, [sa 1 usiku]
Sweden v Bosnia-Hercegovina, [saa 2 usiku]
Ukraine v Romania, [saa 2 na nusu usiku]
United Arab Emirates v Moldova, [saa 2 usiku]
USA v Turkey, [saa 3 usiku]

No comments:

Powered By Blogger