Thursday, 27 May 2010

Pellegrini asikitishwa!
Baada ya kumwaga unga Real Madrid, Manuel Pellegrini, ameelezea masikitiko yake kwa jinsi alivyotendewa na jinsi alivyovunjika moyo kwa kutofanikisha matarajio yake.
Pellegrini alilalamika: “Nlikuja hapa na matumaini makubwa na fahari kubwa ya kuiongoza Timu. Lakini bahati mbaya sikufanikiwa na nilikuwa na tofauti kubwa na Uongozi wa Klabu.”
Pellegrini alitoboa kuwa kulikuwa na tofauti kubwa ndani ya klabu na akatoa mfano wa yeye kutaka Wachezaji Wesley Sneijder na Arjen Robben wabaki Real kwa vile ni wazuri lakini Uongozi ulitaka wauzwe.
Sneijder akatimkia Inter Milan na Robben akatua Bayern Munich.
Bosi huyo wa zamani wa Real anaetoka Chile, alijiunga hapo Mwezi Juni 2009 akitokea Villareal na alitua hapo kumbadili Juande Ramos lakini alishindwa kuiongoza Timu na haikufika hata Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIG, ikatolewa Copa del Rey na Timu ndogo na ikaukosa Ubingwa wa Spain uliochukuliwa na Mahasimu wao FC Barcelona licha ya Klabu kutumia zaidi ya Pauni Milioni 200 kuwanunua Masupastaa Ronaldo, Kaka, Benzema na Alonso.
Pellegrini aliongeza kuwa alikuwa haongei na Rais wa Real Madrid Florentino Perez ambae alizungumza nae kwa mara ya mwisho mwezi Agosti Mwaka jana.
Pelligrini alikiri ameumizwa sana roho kwa jinsi mrithi wake alivyotafutwa na hilo analiona si jambo la utu na si uungwana hata chembe.
Hata hivyo, Pellegrini, amemtakia kila la heri Jose Mourinho.

No comments:

Powered By Blogger