Monday, 24 May 2010

Leo England v Mexico Uwanjani Wembley
Matayarisho ya England kwa ajili ya Kombe la Dunia leo yatapata mtihani Uwanja wa Wembley Jijini London watakapocheza na Timu ngumu Mexico kuanzia saa 4 usiku saa za bongo.
England walikuwa kambini Nchini Austria ambako watarudi tena baada ya mechi hii.
Inategemewa leo Fabio Capello, Kocha wa England, atawapumzisha Mastaa kama kina John Terry, Frank Lampard na Ashley Cole kwa vile walicheza Fainali ya FA Cup wiki moja iliyopita na badala yake watachezeshwa kina Joe Hart, Ledley King, Tom Huddlestone na wengineo ambao hucheza England kwa nadra ili kuwapa nafasi waonekane kabla Kikosi hakijapunguzwa kutoka Wachezaji 30 hadi 23 ifikapo Juni 1 kama inavyotakiwa na FIFA.
Hata hivyo Mexico si Timu ya kuibeza na ikiongozwa na Kocha Javier Aguero pia iko matayarishoni kwa Kombe la Dunia na wapo Kundi A pamoja na Afrika Kusini, Ufaransa na Uruguay.
Mexico inao Wachezaji stadi kama vile Andres Guardado Winga anaechezea Deportivo, Giovani Dos Santos, Mchezaji wa Tottenham aliekopeshwa nje, Carlos Vela wa Arsenal, Guillermo Franco wa West Ham na Mchezaji mpya wa Manchester United, Javier Hernandez maarufu kama Chicharito.
Difensi yao inaongozwa na Rafael Marquez wa Barcelona akishirikiana na Ricardo Osorio.
Vikosi vinategemewa kuwa:
England: Hart, Johnson, King, Ferdinand, Baines, Lennon, Huddlestone, Milner, Gerrard, Crouch, Rooney.
Mexico: Ochoa, Salcido, Marquez, Osorio, Juarez, Guardado, J Dos Santos, Torrado, G Dos Santos, Franco, Blanco
Mnigeria ang’aka kutaka kuinunua Ze Gunners
Bilionea wa Nigeria Aliko Dangote alietangazwa kutaka kununua Hisa za Arsenal za Asilimia 16 amekanusha habari hizo na kudai hana nia hiyo.
Ripoti zilidai Dangote atanunua Hisa za Mama Nina Bracewell-Smith ambae ameziweka sokoni Hisa zake za Asilimia 16 zenye thamani ya Pauni Milioni 160.
Dangote amesema ingawa aliwahi kufanya mazungumzo siku za nyuma kuhusu kuwekeza Klabu ya Arsenal hivi sasa hana nia hiyo.
Dangote anakadiriwa kuwa na Fedha kiasi cha Pauni Bilioni 2.3.
Wadau wakubwa wa Arsenal ni Mmarekani Stan Kroenke mwenye Hisa Asilimia 29.88 na Mrusi Alisher Usmanov mwenye Asilimia 26.29.
Kuuzwa kwa Hisa za Mama Bracewell-Smith kumeibua hisia kuwa Wamiliki hao wakubwa watapigania kununua Hisa hizo ili kuiimiliki Klabu hiyo kwani Sheria zinasema kuwa Mdau mwenye Hisa Asilimia 30 anatakiwa kutoa ofa ya kuinunua Klabu yote.
Hadi sasa Wadau hao, Kroenke na Usmanov, hawajabainisha nia zao.

No comments:

Powered By Blogger