Thursday 27 May 2010

UEFA yaweka kibano kwa Klabu za LIGI KUU
UEFA inategemewa kupitisha sheria mpya ambazo zitazibana sana Klabu za England za Ligi Kuu na huenda ikazifanya zisishiriki Mashindano ya Ulaya kama vile UEFA CHAMPIONS LIGI na EUROPA LIGI.
Sheria hizo zinategemewa kupitishwa Alhamisi Mei 27 na Kamati Kuu ya UEFA na ni mkakati wa dhahiri wa Mfaransa Rais wa UEFA Michel Platini ambae ni mpinzani mkubwa wa Klabu za Uingereza hasa England.
Sheria hizo, ambazo zitaanza kazi rasmi Msimu wa Mwaka 2012/13, zinataka Klabu zipunguze na kuweka kiwango katika Mishahara ya Wachezaji, Klabu ziwe zinajiendesha kwa faida na pia kutopewa ruzuku na Wamiliki wake.
Hivi sasa huko England Klabu nyingi zina Mishahara ya kupindukia ya Wachezaji, nyingi zinaendeshwa kwa hasara na kukumbwa na Madeni makubwa na kadhaa wa kadhaa zinategemea ruzuku za Wamiliki wake ili kujiendesha.
Katika Msimu wa Mwaka 2008/9, ambao Klabu nyingi walikamilisha na kukaguliwa Mahesabu yao, kati ya Klabu 20 za Ligi Kuu, 14 zilipata hasara na moja, Blackburn Rovers, ilipata faida ya Pauni Milioni 3.6 lakini baada ya kupewa mkopo wa Pauni Milioni 5 na Mwenye Klabu, kitendo ambacho kitapingana na Sheria mpya za UEFA.
Klabu nyingi Ligi Kuu zinapewa ruzuku na Wamiliki wao na zinazoongoza kwa hili ni Chelsea na Manchester City ambazo Wamiliki wake Roman Abramovich kwa Chelsea na Koo ya Kifalme ya Abu Dhabi kwa Man City, walifuta Madeni makubwa ya Pauni Milioni 47 kwa Chelsea na Pauni Milioni 93 kwa Man City kwa kutoa ruzuku kwa Klabu zao.
Hilo nalo halitakiwi na UEFA katika sheria mpya za Michel Platini ambazo pia zitawataka Wamiliki wawekeze kwenye Klabu kwa kununua Hisa lakini si kukopesha au kutoa ruzuku na pia kujenga Miundombinu kama Viwanja vya Mazoezi na Vyuo vya kuendeleza Vijana badala ya kuwa wanalipa Mishahara minono kwa Wachezaji au kununua Wachezaji kwa bei mbaya.
Mwenyewe Platini anadai sheria hizi ni suala la kufa na kupona kwa Soka hasa kwa vile Klabu zinakabiliwa na Madeni makubwa.
Katika Ligi Kuu, ukiondoa Chelsea na Man City, Aston Villa walipewa ruzuku na Mmiliki wake lakini walikuwa na hasara ya Pauni Milioni 46 kwa Mwaka 2008/9, Sunderland hasara ya Pauni Milioni 26, Liverpool hasara ya Pauni Milioni 55.
Kwa Manchester United, Mahesabu yao yameonyesha kupata faida kwa sababu tu walimuuza Cristiano Ronaldo kwa dau la Pauni Milioni 81 na kabla ya hapo Klabu hiyo ilikuwa ikionyesha kila Mwaka hasara tu tangu inunuliwe na Familia ya kina Glazer.
Kwenye Vikao vya UEFA, Ligi Kuu ilikuwa ikipigania kwa Klabu zake ziruhusiwe kupokea ruzuku toka kwa Wamiliki wake lakini walishindwa nguvu na Wanachama wengi wa UEFA waliopinga hilo.
Endapo Klabu itashindwa kutekeleza sheria hizo mpya haitaruhusiwa kucheza Mashindano ya Klabu za Ulaya.

No comments:

Powered By Blogger