Monday, 30 August 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com


Mourinho na Real yake mwendo kusuasua, Barca mwendo mdundo!
‘Mtu Spesheli’, Jose Mourinho, jana ameanza himaya yake kwenye La Liga huko Spain akiwa na Real Madrid yake kwa sare ya ugenini ya 0-0 walipocheza na Mallorca ambao walionekana bora zaidi kupita Real.
Mabingwa Barcelona, nao wakicheza awali ugenini, waliifumua Racing Santander kwa bao 3-0 kwa mabao ya Lionel Messi, Andres Iniesta na David Villa.
Ingawa Real kwenye Difensi, iliyokuwa na Beki wa zamani Chelsea Carvalho, walionekana imara, Kiungo na Ushambuliaji wao ulikuwa hafifu.
Mourinho aliwashangaza wengi pale alipowaweka benchi Wachezaji wapya wa Ujerumani waliosainiwa kwa mbwembwe nyingi, Sami Khedira na Mesut Oezil, ingawa waliingizwa baadae lakini hawakubadilisha chochote uwanjani.
TETESI………………..Rodwell kwenda Man United!!!!!!
Baadhi ya Magazeti huko Uingereza yameibua kuwa Nyota Chipukizi wa Everton, Jack Rodwell, yuko njiani kwenda Manchester United kabla Dirisha la Uhamisho kufungwa hapo kesho.
Inadaiwa Man United watatoa ada ya Pauni Milioni 10 pamoja na Kiungo Michael Carrick ambae amekuwa akisuasua Man United.
Rodwell, Miaka 19, ni Mchezaji anaesifiwa kuwa na kipaji kikubwa na mwenye uwezo wa kucheza Kiungo au Sentahafu na Wadau wamemfananisha na Rio Ferdinand alipokuwa mdogo.
Man United wamekuwa wakimfuatilia kwa kipindi kirefu Mchezaji huyo ambae alianza kuichezea Everton tangu akiwa na Miaka 7 na alieweka Rekodi ya kuchezea michuano ya Ulaya ya UEFA akiwa mdogo na umri wa Miaka 16 tu.
Rodwell alianza kucheza mechi za Ligi Kuu Mwaka 2008 na Msimu uliopita alicheza katika mechi ambayo Everton iliifunga Man United 3-1 na yeye kufunga bao moja.
Gyan kwenda Sunderland?
Nyota wa Ghana alieng’ara na pia kuvunja mioyo ya Afrika kwenye Kombe la Dunia, Asamoah Gyan, atahamia Klabu ya Sunderland ikiwa mazungumzo kati ya Rennes ya Ufaransa, Klabu yake ya sasa, na Sunderland yatafanikiwa.
Klabu hizo zina muda hadi kesho ili kukamilisha Uhamisho huo kabla Dirisha la Uhamisho halijafungwa Agosti 31.
Gyan alikosa kufunga penalti dakika ya mwisho ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia Ghana ilipocheza na Uruguay na hatimaye Ghana kubwagwa nje.
Capello ataja England ya EURO 2012
Kocha Fabio Capello ametangaza Kikosi chake cha England kitachocheza Mechi za Makundi za EURO 2012 dhidi ya Bulgaria hapo Ijumaa Septemba 3 na Uswisi Jumanne Septemba 7.
Capello amemrudisha tena kundini Kipa Scott Carson ambae hajaidakia England kwa Miaka miwili na pia kuwaita tena baadhi ya Wachezaji ambao alikuwa hawachagui siku za nyuma za hivi karibuni.
Miongoni mwa hao ni Matthew Upson, Michael Carrick, Shaun Wright-Phillips, Peter Crouch na Jermain Defoe.
Hata hivyo, Mchezaji wa Liverpool, Joe Cole, hakuchaguliwa kinyume cha matarajio ya wengi.
Wengine ambao hawakuchukuliwa kwa sababu ya kuwa majeruhi ni Wachezaji wawili wa Chelsea, John Terry na Frank Lampard, Rio Ferdinand na Bobby Zamora.
KIKOSI KAMILI:
MAKIPA: Scott Carson (West Brom), Ben Foster (Birmingham), Joe Hart (Manchester City).
WALINZI: Gary Cahill (Bolton), Ashley Cole (Chelsea), Michael Dawson (Tottenham), Kieran Gibbs (Arsenal), Phil Jagielka (Everton), Glen Johnson (Liverpool), Joleon Lescott (Manchester City), Matthew Upson (West Ham)
VIUNGO: Gareth Barry (Manchester City), Michael Carrick (Manchester United), Steven Gerrard (Liverpool), Adam Johnson (Manchester City), James Milner (Manchester City), Theo Walcott (Arsenal), Shaun Wright-Phillips (Manchester City), Ashley Young (Aston Villa)
MASTRAIKA: Darren Bent (Sunderland), Carlton Cole (West Ham), Peter Crouch (Tottenham), Jermain Defoe (Tottenham), Wayne Rooney (Manchester United).

No comments:

Powered By Blogger