Wednesday 1 September 2010

PITIA: www.sokainbongo.com

Spurs yamchukua Van der Vaart lakini dili haijabarikiwa
Wasimamizi wa Ligi Kuu bado hawajabariki uhamisho wa sekunde za mwisho wa Staa wa Uholanzi Rafael Van der Vaart kutoka Real Madrid kwenda Tottenham kwa ada ya Pauni Milioni 8.
Awali anga za habari zilidai Van der Vaart, Miaka 27, amehamia Bayern Munich kwa dau la Pauni Milioni 18 lakini Meneja wa Spurs, Harry Redknapp, amedai dili hiyo ilibomoka na yeye kujulishwa masaa mawili kabla uhamisho kufungwa na ndipo alipoamua kumnyakua kwa vile ni Mchezaji wa kiwango cha juu.
Redknapp ametamka: “Ni Mchezaji mzuri na atatoa mchango mkubwa kwetu. Ilikuwa dili ya dakika za mwisho. Asubuhi sikuwa hata na nia ya kumchukua. Nadhani baada ya kushindikana kuhamia Ujerumani ndipo dau lake likaporomoka kadri Dirisha la kufungwa uhamisho lilipokaribia.”
Van der Vaart ni mmoja wa Wachezaji waliocheza na kuisaidia Uholanzi kufika Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini ambako walifungwa 1-0 na Spain.
Kiungo huyo wa Uholanzi alihamia Real Madrid kutoka Hamburg ya Ujerumani Mwaka 2008 lakini uchezaji wake huko Real ulikuwa wa nadra.
Ligi Kuu imesema itatoa tamko lake kuhusu uhamisho huo leo.
Stoke yachota Watatu
Huku dakika zikiyoyoma kabla Dirisha la Uhamisho kufungwa hapo jana, Stoke City ilifanikiwa kuwachukua Wachezaji watatu kwa mpigo ambo ni Eidur Gudjohnsen, Marc Wilson na Jermaine Pennant.
Gudjohnsen, aliewahi kuchezea Chelsea na Barcelona, amechukuliwa kwa mkopo kutoka Monaco na Wilson ametokea Portsmouth ambao pia wamepewa Wachezaji wawili, Liam Lawrence na David Kitson, katika dili hiyo.
Pennant, aliewahi kuzichezea Arsenal, Liverpool, Leeds United na Birmingham, ametua Stoke kwa mkopo kutoka Real Zaragoza ya Spain.
Yobo kuhamia Fenerbahce
Everton imethibitisha kuwa Beki wao kutoka Nigeria Joseph Yobo atahamia Klabu ya Uturuki Fenerbahce kwa mkopo wa Msimu mmoja huku kukiwa na kipengele kuwa Fenerbahce wanaweza kumchukua moja kwa moja baada ya kwisha mkopo huo kwa dau la Pauni Milioni 5.
Yobo, ambae Mkataba wake na Everton unakwisha 2014, amekuwa akichezea hapo kwa Miaka 9 sasa na amecheza mechi zaidi ya 250.
Mnigeria huyo hivi karibuni amekuwa akikosa namba ya kudumu kwani Meneja wa Everton David Moyes amekuwa akiwapanga nafasi za Sentahafu Phil Jagielka na Sylvain Distin huku John Heitinga na Jack Rodwell pia wakiwa na uwezo wa kucheza pozisheni hizo.
Ingawa Dirisha la Uhamisho huko England tayari limefungwa jana huko Uturuki linafungwa rasmi Jumatano Septemba 1.

No comments:

Powered By Blogger