Friday, 3 September 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

England bila Mastaa maarufu kuivaa Bulgaria leo!
• Bulgaria kumchokoza Rooney apande munkari?
England leo inaingia Uwanja wa nyumbani Wembley Jijini London kuivaa Bulgaria katika mechi ya kwanza ya Kundi G ili kuwania nafasi ya kucheza Fainali za EURO 2012 huko Poland na Ukraine, Nchi mbili Wenyeji kwa pamoja, Mwaka 2012.
Lakini England inayoingia leo Wembley ni tofauti na ile England iliyokuwa huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia na kutolewa Raundi ya Pili na Ujerumani kwa kubamizwa 4-1.
Mbali ya majeruhi kadhaa ambao hawakuteuliwa kwenye mechi hii, Wachezaji wengine wamejitoa tayari wakiwa kambini kama vile Kipa Scott Carson wa West Bromwich aliejitoa baada ya kupata msiba kwenye Familia.
Hivyo, imebidi Kocha Fabio Capello amwite Kipa wa Timu ya Vijana wa Chini ya Miaka 21, Scott Loach, kuziba nafasi yake.
Pia Straika Peter Crouch ameondoka baada ya kushindwa kupona tatizo la mgongo.
Wengine ambao waliachwa tangu awali ni John Terry na Frank Lampard, ambao ni majeruhi, David James na Ledley King, ambao wameachwa tu kwa sababu ya viwango, na Jamie Carragher ambae amestaafu kwa mara ya pili sasa.
Wadau wengi wataikodolea macho nafasi ya Masentahafu kwani kwenye mechi hii, Jagelka wa Everton na Matthew Upson wa West Ham, ndio wanaotegemewa kucheza pamoja na hawa hawajahi kucheza pamoja hata mara moja.
Ingawa Capello analijua hilo lakini ameonyesha kutokuwa na wasiwasi pale aliposema Mafulbeki wake Glen Johnson na Ashley Cole watakuwepo kuwasaidia Masentahafu hao.
Pia Capello amedokeza Kikosi chake kwa kuwataja baadhi kama vile Kipa Joe Hart, Wayne Rooney, Steve Gerrard, Gareth Barry, Ashley Cole, Glen Johnson na Jagielka.
Wakati huohuo, Kocha wa Bulgaria, Stanimir Stoilov amesisitiza Bulgaria haitamwinda Wayne Rooney ili kumchokoza ili apandishe hasira ingawa amemtaka Refa wa mechi hiyo kutoka Hungary, Viktor Kassai, awe anazichunga hasira za Rooney.
Wadau, licha ya kushangazwa na kauli ya Stoilov, wamechukulia hilo kama vita ya kisaikolojia.
Carragher: ‘Ubingwa Liverpool hamna!’
• Kesho mechi yake ya kumuenzi Liverpool
Huku kesho akiwa ameandaliwa Mechi maalum kuuenzi utumishi wake Liverpool, Beki Mkongwe wa Liverpool, Jamie Carragher, ameungama kuwa Msimu huu Liverpool haina ubavu wa kuchukua Taji la Ligi Kuu England na badala yake ni bora wapiganie Vikombe tu kama vile Carling Cup na FA Cup.
Msimu uliokwisha Liverpool ilimaliza ikiwa nafasi ya 7 na hiyo ni nafasi ya chini kabisa kwao kumaliza Ligi Kuu tangu ianzishwe.
Carragher, ambae hajawahi kuichezea Klabu yeyote nyingine mbali ya Liverpool na pia hajawahi kuwa Bingwa wa Ligi Kuu, amekiri ni ngumu kwao kushindana na Vigogo kama Chelsea na Manchester United na hata Manchester City, ambao utajiri wao umewafanya walundike Mastaa kibao.
Jumamosi hii, huko Anfield, itafanyika mechi maalum ili kuenzi utumishi wa Jamie Carragher kwa Klabu ya Liverpool kwa kucheza na Kombaini ya Everton, Klabu nyingine kubwa Jijini Liverpool ambao ni Mahasimu wakubwa.
Inategemewa Mastaa wa zamani wa Liverpool, kina Michael Owen, Danny Murphy, Jerzy Dudek, Luis Garcia na Emile Heskey, watavaa tena Jezi za Liverpool pamoja na Carragher katika mechi hiyo.
Kuhusu Michael Owen kurudi tena Liverpool baada ya ‘kuisaliti’ na kwenda kwa Wapinzani wao wa Jadi, Manchester United, Carragher ametamka: “Sidhani kama hilo litawakera Washabiki. Owen ametoa mchango mkubwa kwa Liverpool na aliondoka hapa kwenda Real Madrid huku Mkataba wake ukikaribia kwisha. Alijiunga Man United wakati akiwa na shida ya kujifufua kiuchezaji hivyo yeye kuikataa nafasi kubwa ya kujiunga Klabu kubwa Man United ungekuwa ujinga.”
Carragher pia akafananisha ujio wa Owen kama ule wa Gwiji la Man United, Sir Bobby Charlton, ambae alivaa Jezi ya Liverpool katika mechi ya kumuenzi Mchezaji Mahiri wa Liverpool Tommy Smith na akasema hadhani kwa Owen kuvaa tena Jezi ya Liverpool ni mbaya zaidi ya Bobby Charlton, ambae ni Man United damu ile mbaya, alievaa Jezi hiyo katika tamasha hilo maalum.

No comments:

Powered By Blogger