Saturday 4 September 2010

TEMBELEA: www.sokainbongo.com

Mechi za Yanga v Simba kutoonekana Dar!
Baada ya Serikali kuufunga Uwanja wa Uhuru kwa matengenezo na kugomea Uwanja wa Taifa kutumika na uamuzi wa Simba kuutumia Uwanja wa CCM Kirumba huko Mwanza, Mashabiki wa Magwiji hao wa Soka Tanzania wa Jijini Dar es Salaam watazikosa Mechi za Yanga v Simba Mwaka huu.
Oktoba 16, kwenye Ligi Kuu Vodacom, ni pambano la Simba v Yanga, na kwa vile Simba ndio wameteuliwa Wenyeji, pambano hilo litachezwa ‘nyumbani’ kwa Simba huko CCM Kirumba.
Hivyo Mashabiki wa Dar itabidi wangoje hadi Mwakani waone pambano la Yanga na Simba la marudiano.
Wakati Simba wameshatangaza Uwanja wa nyumbani na kubarikiwa na TFF, Yanga bado hawajasema ‘nyumbani’ ni wapi ingawa inasadikiwa itakuwa ni Uwanja wa Jamhuri huko Morogoro au Sheikh Amri Abeid huko Arusha.
Mfungaji ‘Hetriki’ Defoe amsifia Rooney
• Gwiji Wright ampongeza Defoe!
Mfungaji wa bao 3, Jermaine Defoe, aliepachika bao hizo hapo jana Uwanjani Wembley katika ushindi wa 4-0 wa England dhidi ya Bulgaria kwenye pambano la EURO 2012, amemsifia Wayne Rooney ambae ndie alikuwa mpishi mkuu wa bao zote 4 za England.
Defoe amekuwa Mchezaji wa kwanza wa England kufunga bao 3, ‘hetriki’, Uwanjani Wembley tangu ufunguliwe baada ya kujengwa upya na hivyo kufanya magoli yake kwa England kuwa 15 katika Mechi 44.
Mchezaji wa mwisho wa England kufunga bao 3 Uwanjani Wembley ni Alan Shearer Mwaka 1999 katika Mechi ya England na Luxemborg.
Defoe, ambae nusura aikose mechi kama asingeahirisha kufanyiwa operesheni ya nyonga, amefurahia mafanikio yake kwa kutamka: “Ni ngumu kuelezea furaha yangu…..huu ni usiku mtamu katika maisha yangu ya Soka! Ukicheza na Mchezaji Bora Rooney na ukiwa mjanja kuingia kwenye nafasi basi atakupata tu kwa pasi murua! Baada ya kufunga bao la pili, Rooney aliniambia ‘nenda kafunge la 3’! Kuambiwa hivyo na Mchezaji mahiri ni kitu poa sana!”
Defoe alitoboa pia kuwa kabla ya mechi aliambiwa na Gwiji la zamani la Arsenal na England, Ian Wright, kwamba wakati wake kufunga bao 3 umefika na baada ya mechi Wright alimtumia Defoe ujumbe wa simu uliosema: “Nakupenda JD, hongera kwa kazi njema!”
Wenger apona rungu la FA
Chama cha Soka England, FA, kimeamua kutomchukulia Arsene Wenger hatua yeyote kwa madai yake Stoke City ni Wacheza Raga kufuatia malalamiko rasmi ya Stoke City.
Meneja huyo wa Arsenal, akionyesha bado kukerwa na Mchezaji wa Stoke Ryan Shawcross kumvunja mguu Chipukizi wa Arsenal Aaron Ramsey mapema Mwaka huu, aliwafananisha Stoke na Wacheza Raga kwa uchezaji wao katika mechi na Tottenham ya Ligi Kuu Mwezi uliokwisha waliyofungwa 2-1.
Kauli hizo za Wenger zilimkera Meneja wa Stoke, Tony Pulis, alielalamika: “Tumesikitishwa na kauli ya Wenger. Haikustahili hata kidogo.”
Pulis, akihojiwa zaidi kuwa anaonaje pengine kumtaja Shawcross katika mechi na Tottenham huku Refa akiwa Chris Foy ambae ndie alichezesha pambano hilo na pia atachezesha la Blackburn na Arsenal ilikuwa mbinu ya Wenger ili wapate imani ya Refa huyo katika mechi yao na Blackburn, Pulis alijibu: “Ni wewe umesema kuwa alitaka kumrubuni Refa awasaidie na mimi nakubaliana na wewe!”
Pulis akaongeza: “Yeye ana uhuru wa kusema atakalo. Sisi tumepigana Vita Kuu mbili za Dunia kulinda uhuru huo! Lakini kile alichosema kuhusu Shawcross ni kitu kibaya na sisi tutamshitaki.”
Hata hivyo, FA imeamua kuwa kwa vile Wenger hakumtaja Refa Foy kwa jina na alikuwa akitoa maoni yake kwa ujumla hana kesi yeyote ya kujibu.

No comments:

Powered By Blogger