Saturday, 4 September 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

FRANCE: Jahazi latota!
• Kocha Blanc anung’unika hana Wapiga Mabao!!
Kocha wa Ufaransa, Laurent Blanc, ambae jana alisimamia Nchi hiyo kwa mara ya kwanza katika Mashindano rasmi na kuaibishwa kwa kuchapwa bao 1-0 nyumbani na Belarus kwenye Mechi ya Makundi kuwania kuingia Fainali za EURO 2012, amenung’unika na kusikitikia kutokuwa na Wachezaji wenye uwezo wa kufunga.
Kipigo hicho cha Belarus kimeendeleza maafa kwa Ufaransa ya toka huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambazo France ilitupwa nje Raundi ya Kwanza kwa kushika mkia Kundi lao na pia Timu kukumbwa na Skandali la ugomvi kambini, mgomo wa Wachezaji, kufukuzwa kwa Nicolas Anelka na hivi juzi sakata hilo likazaa kufungiwa baadhi ya Wachezaji.
Baada ya mechi ya jana, Blanc alisema: “Hatuwezi kusema tunao Wachezaji wanaojua kufunga. Tunao Wachezaji wanaojua kumiliki mpira lakini hatuna wale wenye kuleta mafanikio katika Mita 25 za mwisho.”
Hata hivyo, Banc amekiri Wachezaji wake wana morali ndogo kufuatia maafa ya Kombe la Dunia na Skandali lililofuata baada ya hapo.
Jumanne, Septemba 7, Ufaransa itasafiri kwenda kucheza na Bosnia kwenye mechi ya pili ya Makundi ya EURO 2012 huku Mastraika wake watatu wakiwa majeruhi.
Wachezaji hao ni Louis Saha, Loic Remy na Karim Benzema.
FIFA yageuka!
FIFA imefungua milango wazi kwa Wanachama wake, yaani Vyama vya Soka vya Nchi, kutumia ushahidi wa mikanda ya video ili kupata ushahidi na kuwahukumu Wachezaji wanaovunja sheria kwa kumhadaa Refa ili kupata penalti au kupata maamuzi yanayowafaa.
Miaka miwili iliyopita SFA, Chama cha Soka cha Scotland, kilitoa pendekezo la kutumia video lakini FIFA ikalipinga hilo kwa kutamka kuwa sheria zilizokuwepo halikubali hilo na kwamba uamuzi wa Refa ni wa mwisho.
Lakini, katika uamuzi uliofungua milango, FIFA imekiruhusu Chama cha Soka huko Australia kuwafungia Wachezaji wawili waliojiangusha kwa kusudi na kupata penalti na baadae ushahidi wa video ulionyesha walidanganya.
Huko Ulaya, UEFA tayari ilishatumia video kumhukumu Mchezaji aliemhadaa Refa na kupata penalti na baada ya mechi hiyo Mchezaji huyo, ambae alikuwa Eduardo wa Arsenal, akafungiwa mechi.

No comments:

Powered By Blogger