Saturday 27 February 2010

FAINALI : Safari ya Wembley
Fainali ya Kombe la Carling ni Jumapili Februari 28 Uwanja wa Wembley kati ya Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo Manchester United na Aston Villa na mechi hii itaanza saa 12 jioni saa za bongo chini ya usimamizi wa Refa Phil Dowd.
Safari ya Timu hizi kufika Wembley ilianza Raundi ya 3 na mechi zao zilikuwa:
RAUNDI YA 3
Man United 1 Wolves 0
Aston Villa 1 Cardiff 0
RAUNDI YA 4
Barnsley 0 Man United 2
Sunderland 0 Aston Vill 0 [Villa walishinda 3-1 kwa penalti]
ROBO FAINALI
Portsmouth 2 Aston Villa 4
Man United 2 Tottenham 0
NUSU FAINALI
-Mechi za kwanza
Manchester City 2 Man United 1
Blackburn 0 Aston Villa 1
-Mechi za marudiano
Man United 3 Man City 1
Aston Villa 6 Blackburn 4
NI FAINALI!!!!
Wakati Martin O'Neill bado anasaka Kombe tangu aanze kazi ya Umeneja Aston Villa ingawa aliwahi kuvitwaa Vikombe viwili alipokuwa Leicester City, Manchester United ndio Mabingwa Watetezi wa Kombe hili la Carling baada ya kulitwaa msimu uliopita walipowabwaga Tottenham kwa penalti.
Aston Villa kama Klabu mara ya mwisho kuchukua Kikombe ni mwaka 1996 walipotwaa Kombe la Ligi ambalo sasa ndio Carling walipowatoa Leeds United Fainali.
Msimu huu, Aston Villa na Manchester United zimecheza mara mbili na Villa walishinda Old Trafford 1-0 na hivi majuzi walitoka sare 1-1 Villa Park huku Man United ikicheza mtu 10 kwa karibu saa nzima baada ya Winga wao Nani kupewa Kadi Nyekundu.
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, amekuwa akichezesha Chipukizi kwenye mechi za Raundi za mwanzo za michuano hii lakini walipofika Nusu Fainali na kukutana na Mahasimu wao wakubwa Manchester City aliweka Wachezaji wazoefu.
Akizungumzia Fainali, Ferguson alisema: “Kucheza Wembley ni tukio kubwa. Lakini utaiskia raha tu ya kucheza Wembley ukishinda! Tuna nafasi ya kushinda!”
Nae Martin O’Neill, Meneja wa Aston Villa, anasema: “Hapa Klabuni, tuna picha nyingi za Timu zetu za zamani zilizobeba Vikombe! Sisi je? Mafanikio ya Timu hizo ni changamoto kwetu na tunataka kushinda!”
Ingawa msimu huu Aston Villa wamegangamara kwa Manchester United lakini katika mapambano 37 kati yao Villa wameshinda mara mbili tu.
Wakati Villa haina majeruhi, Manchester United itawakosa majeruhi Rio Ferdinand, Ryan Giggs na Anderson, na Nani hawezi kucheza kwani yuko kifungoni mechi 3 kwa kupewa Kadi Nyekundu mechi ya Ligi na Aston Villa.
Vikosi vinategemewa:
Aston Villa (4-4-2): Friedel; Cuellar, Dunne, Collns, Warnock; A Young, Milner, Petrov, Downing; Agbonlahor, Heskey.
United: (4-4-2) Foster; Neville, Vidic, Brown, Evra; Scholes, Fletcher, Carrick, Park; Rooney, Berbatov.
Refa: Phil Dowd.

No comments:

Powered By Blogger