Tuesday 23 February 2010

Nyota wa Everton toka Bondeni abambwa akiwa njwiiii!!!
Kiungo wa Everton anaetoka Afrika Kusini Steven Pienaar amekamatwa akiendesha gari huku akiwa amelewa chakari asubuhi ya Jumapili.
Pienaar, miaka 27, aliichezea Everton Jumamosi walipoifunga Manchester United 3-1 kwenue Ligi Kuu.
Pienaar sasa atapanda kizimbani Machi 9 kujibu mashitaka dhidi yake.
Anderson njia panda Man United?
Huenda siku za Anderson kubakia Manchester United zimeanza kuhesabiki baada ya kuwa na matatizo na Meneja wake Sir Alex Ferguson kitu ambacho kimefanya Kijana huyo toka Brazil akose namba kwa Mabingwa hao.
Mechi ya mwisho kwa Anderson kuichezea Man United ni Januari 19 alipokuwemo kwenye Kikosi kilichofungwa 2-1 na Manchester City kwenye Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Carling.
Inadaiwa Ferguson alimfokea Anderson kwa kucheza chini ya kiwango katika mechi hiyo na akamtema katika mechi iliyofuata Man United waliyocheza na Hull City na hilo likamkasirisha Anderson alietimkia kwao Brazil bila ruhusa ya Klabu.
Si Anderson wala Ferguson waliozungumza chochote kuhusu madai hayo ya mfarakano kati yao ila mwenyewe Anderson amesisitiza yeye matumaini yake bado yapo Man United na anachotaka ni namba ya kudumu ili Kocha Dunga wa Brazil amchukue kwenye Kombe la Dunia.
SKANDALI LA TERRY: Bridge & Terry si tatizo kuwa England!!!
Mmoja wa Wasaidizi wa Kocha wa England Fabio Capello, Stuart Pearce anaamini kuwa hakutakuwa na tatizo lolote kwa John Terry na Wayne Bridge kuichezea England pamoja baada ya Terry kukumbwa na kashfa ya kutangazwa kutembea na gelfrendi wa Bridge sakata ambalo limemfanya Capello amtimue Unahodha wa England.
Capello anategemewa kutangaza Kikosi cha England kitakachocheza mechi ya kirafiki na Misri Jumatano ijayo wikiendi hii na Wachezaji hao wawili huenda wakawemo.
Uteuzi wa Wayne Bridge kwa England ni kitu kisichoepukika hasa kwa vile Beki wa kushoto wa kutumainiwa Ashley Cole ni majeruhi.
Hata hivyo Wachezaji hao wanaweza wakakutana Uwanjani kabla ya kuwa Kikosi cha England kwa vile Klabu ya Terry Chelsea itacheza na Klabu ya Bridge Manchester City Jumamosi huko Stamford Bridge kwenye Ligi Kuu.
Stuart Pearce amesisitiza kuwepo pamoja Wachezaji hao si tatizo kwani kuichezea England ni kitu muhimu sana kuliko ubinafsi na wote, Terry na Bridge, ni Wachezaji thabiti wa kulipwa wanaoheshimu maadili ya kazi yao.

No comments:

Powered By Blogger