Thursday 25 February 2010

Mourinho atamba kuingia Robo Fainali UEFA!
Kocha wa Inter Milan Jose Mourinho baada ya kuifunga Chelsea 2-1 hapo jana Uwanjani San Siro amejigamba kuwa wao wataingia Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI na hana wasiwasi na mechi ya marudiano Machi 16 huko Stamford Bridge.
Mourinho ametamba: “Mourinho hafungwi Stamford Bridge!”
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kurudi Stamford Bridge kwa Mourinho tangu aihame Klabu hiyo Septemba 2007 na amesema mechi ya marudiano mabao si muhimu bali ni matokeo tu yatakayomfanya asonge mbele.
Pia Mourinho allikiri kuwa katika mechi ya jana Chelsea walistahili kupata penalti kipindi cha kwanza.
Wayne Bridge ajitoa kuchaguliwa England
Wayne Bridge ametangaza kuwa hawezi kuwepo katika uteuzi wa Wachezaji watakaounda Kikosi cha England kitakachocheza mechi ya kirafiki Machi 3 na Misri.
Kocha wa England Fabio Capello anatarajiwa kufanya uteuzi huo Jumapili lakini Bridge amejitoa kwa kusema si muafaka na pengine uteuzi wake utaigawa England hasa ukizingatia skandali la John Terry ambae alivuliwa Unahodha wa England kwa kuhusishwa na kutembea na gelfrendi wa Wayne Bridge.
Uteuzi wa Bridge kwenye Timu ya England ulikuwa ni wazi hasa baada ya kuumia kwa Beki wa kushoto wa kudumu wa Timu hiyo Ashley Cole.
Hata hivyo Wayne Bridge na John Terry watakuwa Uwanja mmoja siku ya Jumamosi pale Klabu ya Terry Chelsea itakapovaana na Manchester City Klabu ya Bridge huko Stamford Bridge kwenye mechi ya Ligi Kuu.
Anderson nje msimu wote!
Kiungo kutoka Brazil wa Manchester United Anderson amepata pigo kubwa kwa kuumia goti litakalomuweka nje ya uwanja msimu wote na hivyo kulikosa Kombe la Dunia ambalo alikuwa na matumaini makubwa kuchukuliwa na Brazil.
Anderson aliumia dakika ya 19 ya mchezo kati ya Manchester United na West Ham ambapo Man United walishinda 3-0 hapo juzi Jumanne Uwanjani Old Trafford.
Vile vile, Rio Ferdinand yupo nje kwa kuuumia tena mgongo ambao umekuwa ukimsumbua muda mrefu.
Ni majuzi tu Rio alirudi kucheza tena baada ya kukaa nje miezi mitatu kwa kuumwa mgongo lakini alicheza mechi moja tu na akapata mkosi wa kufungiwa mechi 4 kwa kupatikana na hatia ya kumpiga Craig Fagan wa Hull City Man United ilipocheza na Timu hiyo.
Rio ataikosa Fainali ya Carling Cup hapo Jumapili Manchester United watakapokumbana na Aston Villa na pia mechi ya kirafiki ya England na Misri Jumatano ijayo ambayo ndio ingekuwa mechi yake ya kwanza kama Kepteni wa England baada ya kutimuliwa John Terry.
Lakini Meneja wake Sir Alex Ferguson ana mategemeo makubwa Rio safari hii atarudi uwanjani mapema.

No comments:

Powered By Blogger