Tuesday 23 February 2010

ISHARA YA PINGU YAMPA KIFUNGO MOURINHO
Jose Mourinho, Meneja wa Inter Milan, amefungiwa mechi 3 na kutwangwa faini ya Euro 40,000 kufuatia kitendo chake cha kutoa ishara ya pingu kwa mikono yake katika mechi ya Ligi Serie A ya Jumamosi waliyotoka sare 0-0 na Smpdoria na ambayo Wachezaji wa Inter Milan wawili walitolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
Mabeki wa Inter Walter Samuel na Ivan Cordoba walipotolewa ndipo Mourinho akatoa ishara ya pingu akionyesha Timu yake inaonewa na Marefa.
Kitendo hicho cha pingu kinafuata kauli yake aliyoitoa siku moja kabla ya mechi hiyo ya Jumamosi aliposema: “Hapa Italia kuna Timu moja yenye eneo la penalti refu kupita nyingine!”
Mreno huyo alikuwa akiimaanisha Juventus wakati Fowadi wao Alessandro Del Piero alipochezewa rafu nje ya boksi na ikatolewa penalti. Mourinho amekuwa akisakamwa sana huko Italia kwa kauli na vitendo vyake.
Kifungo cha Mourinho kitamfanya azikose mechi za Serie A dhidi ya Udinese, Genoa na Catania na Wachezaji wake Sulley Muntari na Cambiasso wamefungiwa mechi 2 kila mmoja kwa rabsha kwenye mechi hiyo hiyo na Sampdoria iliyomfunga Mourinho.
Wachezaji, Samuel na Cordoba, kwa Kadi Nyekundu katika mechi hiyo watakosa mechi moja.
Inter Milan bado wapo kileleni mwa Ligi kwa pointi 5 mbele ya AS Roma.
TATHMINI: UEFA CHAMPIONS LEAGUE
[mechi zote saa 4 dak 45 usiku isipokuwa inapotajwa]
Jumanne, Februari 23
Stuttgart v Barcelona
Olympiakos v Bordeaux
Jumatano, Februari 24
CSKA Moscow v Sevilla [saa 2 na nusu usiku]
Inter Milan v Chelsea
Hii ni wiki ya pili ya mechi za UEFA CHAMPIONS LIGI baada ya mechi 4 za wiki iliyopita za Raundi ya Mtoano ya Timu 16.
Bila shaka, Bigi Mechi ya wiki hii ni ile ya San Siro kati ya Inter Milan na Chelsea ambayo wengi wameibatiza Mourinho v Chelsea kwa vile tu Meneja wa Inter Milan Jose Mourinho alikuwa Bosi wa Chelsea kabla ya kuhamia Inter Milan.
Timu hizo, Inter Milan na Chelsea, hazijawahi kukutana kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI lakini Mameneja wao wanazijua Timu pinzani vilivyo huku Mourinho akiijua Chelsea nje ndani na Carlo Ancelotti lazima ataijua Inter Milan kwa vile tu alikaa misimu minane kwa Wapinzani wa Inter, AC Milan.
Chelsea na Inter ndizo zinazoongoza Ligi zao kwa sasa.
Inter Milan msimu uliokwisha waling’olewa kwenye hatua hii ya UEFA na Manchester United walipopigwa jumla ya bao 2-0.
Mabingwa Watetezi wa UEFA CHAMPIONS LIGI, Barcelona watakuwa Ujerumani kucheza na Stuttgart bila ya Wachezaji Mabeki Eric Abidal na Dani Alves na Viungo Xavi Hernandez na Syedou Keita walio majeruhi.
Wakati Barcelona ndio wanaongoza Ligi yao La Liga, Stuttgart wanaelea katikati kwenye msimamo wa Bundesliga ingawa mechi yao ya juzi waliishindilia Cologne bao 5-1.
Kwenye mechi na Barcelona, Stuttagrt wakiongozwa na Kocha Christian Goss watawakosa Wachezaji wao Ciprian Marica, Arthur Boka na Sami Khedira.
Bordeaux, ambao wako ugenini huko Ugiriki kucheza na Olympiakos, wanaingia kwenye mechi hii ya Jumanne wakiwa na rekodi nzuri kwenye mechi zao za Makundi za Mashindano haya pale waliposhinda mechi 5, sare moja na kufungwa goli 2 tu.
Olympiakos sasa wako chini ya Kocha Bozidar Bandovic aliechukua hatamu toka kwa Zico wa Brazil na wao walimaliza mechi zao za Makundi wakiwa nyuma ya Arsenal na walishinda mechi zao zote za nyumbani bila kufungwa hata goli moja.
CSKA Moscow hawajacheza hata mechi moja tangu Novemba msimu wa Ligi ya Urusi ulipomalizika na wanawakaribisha Sevilla Jumatano.
Hata hivyo, pengine silaha kubwa ya CSKA kwenye mechi hii na Sevilla ni baridi kali itakayowakumba Sevilla.
Katika msimu wa Ligi ya Urusi uliokwisha Novemba, CSKA wamemaliza Ligi hiyo wakiwa nafasi ya 5.
Kwenye Makundi ya Mashindano haya, CSKA walimaliza nyuma ya Manchester United na kuzipiku Wolfsburg na Besiktas.

No comments:

Powered By Blogger