Friday 26 September 2008

Joe Kinnear ateuliwa Meneja wa muda NEWCASTLE

Tangu Kevin Keagan aachie ngazi Newcastle tarehe 4 Septemba 2008, Klabu hiyo imekuwa haina Meneja na timu ilikuwa chini ya uongozi wa aliekuwa kocha msaidizi Chris Hughton huku Menejimenti ikiyumba na kujikuta ikiwa na mzozo mkubwa na mashabiki wa timu hiyo waliochukua hatua ya kuandamana kupinga kuondoka Kevin Keagan.
Maandamano hayo yalimuudhi sana mmiliki wa Klabu Mike Ashley ambae akaamua kuiuza klabu hiyo. Hivi sasa yuko kwenye pilipilika za kuiuza huku kuna tetesi kwamba kuna Kampuni moja kubwa toka Nigeria imetoa ofa ya kuinunua ingawa habari nyingine zinasema mwenye klabu Mike Ashley anatafuta mnunuzi toka Arabuni.
Wakati mizozo na wasiwasi ukiendelea timu nayo imekuwa haifanyi vizuri uwanjani na imeshapata vipigo vitatu mfululizo tangu kuondoka Kevin Keagan hali iliyomfanya Kocha msaidizi Chris Hughton kutaka uongozi wa Klabu kutafuta Meneja wa kudumu.
Leo Menejimenti imemtaja Joe Kinnear, umri miaka 61, [pichani]kuwa Meneja wa muda mpaka mwishoni mwa Oktoba inapotegemewa klabu hiyo itakuwa ishauzwa.
Joe Kinnear, raia wa Ireland, mara ya mwisho alikuwa Meneja wa Nottingham Forrest kazi aliyojiuzulu Desemba 2004 na tangu wakati huo hajaongoza timu nyingine yeyote.
Kabla ya hapo alishakuwa Meneja wa Wimbledon na baadae Luton.
Nae Chris Hughton aliekuwa akiongoza timu ameukaribisha uteuzi huo kwa kutamka kuwa Joe Kinnear ni mzoefu sana na atasaidia klabu katika wakati huu mgumu.

No comments:

Powered By Blogger