Tuesday, 23 September 2008

Sir Alex Ferguson: Sasa subirini muone tukipaa!!!


Mashetani Wekundu Manchester United huenda wakawa wameuanza msimu polepole lakini Meneja wao Sir Alex Ferguson anasisitiza vimbwanga vyao vitaanza kuonekana wakati wowote kuanzia sasa.
Suluhu ya 1-1 na Chelsea siku ya Jumapili huko Stamford Bridge imewafanya wawe na pointi 5 kwa mechi 4 walizocheza lakini Ferguson ana uhakika hamna haja ya kuingiwa hofu.
'Tulikuwa na mwanzo mgumu,' Ferguson alitamka. 'Ilibidi tucheze ugenini Anfield na tulipoteza mchezo ule na Liverpool kwa kuwapa zawadi ya magoli mawil! Sasa ikabidi twende tena ugenini Stamford Bridge! Lakini tumecheza ugenini Portsmouth na kushinda
na naamini hapo Portsmouth timu nyingi zitakwama kwani ni wagumu sana kwao!'
Akaongeza: 'Ni vigumu kusema hii dro ya 1-1 na Chelsea itatufikisha wapi lakini ikifika Oktoba watu wataona Man U iko wapi- ni juu inapostahili!'
Mechi za Man U za LIGI KUU zinazofuata ni na Bolton Jumamosi hii hapo Old Trafford kisha na Blackburn, ikifuatiwa na West Brom, halafu na Everton na ya mwisho kwa mwezi Oktoba ni ya West Ham.
Ferguson aliendelea kufafanua: 'Wachezaji wengi waliokuwa majeruhi watapata mazoezi zaidi na kuwa fiti zaidi. Ronaldo na Berbatov ambao hawajacheza mechi nyingi msimu huu watakuwa wameshajijenga vizuri.'
Sir Alex Ferguson pia aliponda magazeti mengi yaliyoandika kwamba endapo Man U watafungwa na Chelsea basi watakuwa pointi 9 nyuma.
Alidai hawa wapuuzi wanasahau Man U wamecheza mechi moja pungufu.
Leo usiku saa 4 [bongo taimu] Manchester United wanaingia kwao Old Trafford kupambana na Middlesbrough kwenye mpambano wa kuwania Kombe la Carling. Ferguson ameahidi kushusha kikosi mchanganyiko wa chipukizi na mastaa ambao hawajacheza mechi nyingi msimu huu.
Amewataja Owen Hargreaves, Ji-sung Park, Nani, Anderson na Cristiano Ronaldo wote watakuwa kwenye kikosi kwa kuwa wanahitaji mechi ila kuwa fiti zaidi. Chipukizi wanaoweza kuwemo pia ni Jonny Evans, Darron Gibson, Danny Welbeck na Rafael.
Alisikitika kwamba Muangola Manucho hawezi kucheza kwani hajapona sawasawa mfupa wa kidole alichovunjika mazoezini.

No comments:

Powered By Blogger