Monday 15 February 2010

Bosi wa Palace ataka Mshika kibendera afungiwe!
Meneja wa Crystal Palace Neil Warnock ametaka afungiwe Refa Msaidizi Trevor Massey ambae alishika kibendera katika mechi ya jana ya FA Cup kati ya Crystal Palace na Aston Villa iliyoisha 2-2 baada ya Villa kusawazisha bao dakika ya 87 kufuatia kona ambayo Mchezaji alietoa mpira nje alikuwa ni wa Villa na hivyo ilipaswa kuwa golikiki badala ya kona.
Warnock amelalamika: “Goli lao la pili ni aibu! Tumetoka jasho na kupigana kufa na kupona na mwisho tunauawa kwa uzembe wa mtu! Nimeambiwa ikiwa Massey alikosea atasimamishwa lakini hilo linatusaidia nini?”
Sasa Aston Villa na Crystal Palace itabidi zirudiane huko Villa Park tarehe 24 Februari.
Warnock aliendelea kulalama: “Nilimwambia akatizame video na ataona kosa lake! Siwezi kusema zaidi kwani wanasikiliza na sitaki kupoteza pesa zangu kwa kulipa faini! Lakini huu ni wizi!”
Kwa Crystal Palace, ingawa wataona wameonewa kwa mechi kurudiwa, lakini ni bora kwao kifedha kwani Klabu hiyo ipo mikononi kwa Mfilisi kwa vile ina matatizo ya kifedha.
Mshindi kati ya Aston Villa na Crystal Palace atacheza na mshindi kati ya Reading au West Bromwich katika Robo Fainali ya Kombe hili la FA.

No comments:

Powered By Blogger