Friday, 19 February 2010

Togo kuendelea kusota kifungoni
CAS, Mahakama ya Usuluhishi Michezoni [CAS: Court of Arbitration of Sports], imetupilia mbali matakwa ya Togo ya kutofungiwa kucheza Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yajayo mawili na imesema kifungo hicho kinabaki palepale hadi uamuzi kamili wa kifungo cha Togo utakapotolewa na Mahakama hiyo iliyo Mjini Lausanne, Uswisi.
Uamuzi wa CAS unamaanisha Togo haitakuwemo kwenye Droo ya Jumamosi ya kupanga mechi za awali za mtoano za Kombe la Afrika zitazoanza kuchezwa Septemba mwaka huu.
Hata hivyo CAS imetamka kuwa endapo Togo watashinda kesi yao na kufunguliwa na CAS basi CAF itabidi waipange Togo kwenye mechi hizo za Kombe la Afrika.
CAF iliifungia Togo kutoshiriki kucheza Mashindano mawili yajayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada kujitoa Fainali za Kombe hilo zilizofanyika Nchini Angola mwezi Januari.
Togo walijitoa kufuatia maafa waliyoyapata ya kushambuliwa wakati wakisafiri kutoka Congo na kuingia Angola Jimbo la Cabinda na ndipo Basi lao likapigwa risasi na Waasi wa Cabinda na kumuua Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa msafara wa Togo.
Serikali ya Togo ikaamrisha Kikosi chake kirudi nyumbani na CAF imeuchukulia uamuzi huo kama Serikali kuingilia masuala ya Soka na hivyo kuwafungia.
Wadau wengi wanahisi adhabu hii kwa Togo haikustahili ukichukulia misingi ya ubinadamu.

No comments:

Powered By Blogger