• Wavaa Kijani na Dhahabu ishara ya upinzani!!
Hivi karibuni katika kila mechi ya Manchester United, rangi za kijani na dhahabu zimekuwa zikionekana miongoni mwa Washabiki wa Klabu hiyo na hizi ni rangi za Klabu ya Newton Heath iliyoanzishwa mwaka 1878 na hapo tarehe 26 Aprili 1902 kubadilishwa jina kuitwa Manchester United na rangi kuwa nyekundu, nyeusi na nyeupe.
Newton Heath ilianzishwa na Wafanyakazi wa Depo iliyokuwepo Newton Heath la Reli ya Lancashire na Yorkshire..
Mwaka 2005 Familia ya Matajiri kutoka Florida Marekani iitwayo Glazer iliinunua Manchester United na kuiingiza kwenye deni kubwa ambalo, ingawa Menejimenti ya Klabu inadai hilo deni ni kitu cha kawaida na uwezo wa kulilipa upo, Washabiki hawapendeziwi nalo na wameanzisha upinzani mkubwa kwa Familia ya Glazer.
Ndio maana Mashabiki, kwenye mechi za Manchester United, wanavaa skafu, fulana na kofia rangi za kijani na dhahabu ikiwa ni alama ya chimbuko la Manchester United, Klabu ya Newton Heath iliyoanzishwa na Wafanyakazi makabwela wa Depo ya Reli.
Nje ya Uwanja wa Old Trafford fulana za rangi hiyo ya kijani na dhahabu huuzwa huku nyuma zina maandishi [Shairi la Kiingereza] na tafsiri ya haraka ni:
Hatutavaa ile Jezi Nyekundu inayosifika, Mpaka Glazer waondoke au wafe,
Hivyo inua viwango vya zamani juu, Kwa Kijani na Dhahabu tutaishi na kufa,
Na hakika siku itafika tena, Tutakapovaa Nyekundu yetu kwa mara nyingine tena!”
Upinzani huu wa Washabiki umepamba moto na sasa kuna habari kwamba kuna Kikundi cha Matajiri ambao ni Mashabiki wa Manchester United wameanzisha umoja ili kuing’oa Klabu hiyo mikononi mwa Familia ya Glazer.
Matajiri hao wanafanya mikakati na kukusanya uwezo ili kuinunua Klabu hiyo.
Nae Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, akizungumzia sakata hilo la Mashabiki amesema anaelewa uchungu wa Mashabiki ingawa amekiri wale walio madarakani wanafanya kila lililo sahihi kwa maendeleo ya Klabu hiyo.
Inasemekana Mashabiki wanajikusanya ili kufanya maandamano huku kila mtu akivaa kijani na dhahabu kabla ya mechi ya Machi 10 ya marudiano ya UEFA CHAMPIONS LIGI na AC Milan Uwanjani Old Trafford.
Ferguson amesema: “Hilo halinihusu. Hatujali wanavaa rangi gani kwani wote bado wanaisapoti Timu moja tu! Hili linaonyesha Mashabiki wana uchungu na Timu yao!”
Ferguson ameongeza: “Kila Shabiki ana haki ya kulalamika kwa kile wanachoona ni haki lakini inabidi na sie tuiendeshe Klabu kwa njia sahihi. Misingi ya Klabu hii bado ni mizuri! Tuna Timu ya Vijana nzuri na Timu ya kwanza inafanya vizuri sana! Sisi tunaendelea na upande wa soka na wao waendelee tu mradi hawaathiri Timu.”
No comments:
Post a Comment