Saturday 20 February 2010

Wenger kulikwaa rungu la UEFA?
Huenda Meneja wa Arsenal Arsene Wenger akazivaa hasira za UEFA baada ya kumshambulia Refa Martin Hansson aliechezesha mechi yao ya UEFA CHAMPIONS LIGI waliyofungwa na FC Porto bao 2-1 Jumatano huko Ureno kwa kuikubali frikiki tata ya FC Porto iliyozaa bao la ushindi.
Refa Martin Hansson si mgeni kwa migogoro kwani ndie Refa ‘alieibeba’ Ufaransa kuingia Fainali za Kombe la Dunia pale alipogeuka ‘kipofu’ wakati Thierry Henry akiukontroli mpira kwa mkono na kumpasia William Gallas aliesawazisha bao na kuwang’oa Ireland.
Arsene Wenger amemwita Refa huyo hana uwezo wa kuchezesha na hilo linaweza kumtia matatani na UEFA na huenda akashitakiwa na kufungiwa.
Wenger amesema: “Naaminini Refa pengine hana uwezo au si mwaminifu. Lakini ningependa kuamini hana uwezo. Utachukuaje mpira na kumpa Mchezaji na kisha kumwambia funga goli?”
Wenger amedai Refa huyo katika maamuzi yake kuhusu frikiki hiyo iliyozaa goli alifanya makosa matano ya kiufundi ambayo hayakubaliki kwenye mashindano makubwa kama UEFA.
Wenger ameyataja makosa hayo ya Refa kuwa:
-Hakutoa frikiki pale ilipotendeka.
-Hakusimama pale Refa anatakiwa kusimama.
-Hakupanga ukuta katika umbali unaotakiwa.
-Hakupaswa kutoa idhini ya kupigwa frikiki ya haraka wakati yeye mwenyewe yuko katikati ya tukio hilo la kupigwa frikiki.
-Hakunyosha mkono kwa wakati kuashiria sio frikiki ya moja kwa moja [kuwa ni indirect freekick].
Baadhi ya Wadau wamekumbusha ile hadithi ya mkuki kwa nguruwe kwani Arsenal washawahi kunufaika kwa frikiki za aina hiyo hiyo pale Thierry Henry alipofunga magoli mawili dhidi ya Chelsea kwa frikiki za haraka haraka kabla watu hawajajipanga.
Fergie amtaka Scholes aongeze mkataba
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson anataka Paul Scholes aachane na fikra za kustaafu na aongeze mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi.
Mkataba wa Scholes unakwisha Juni mwaka huu na mwaka jana Scholes alitamka kuwa msimu huu, pengine, ndio wa mwisho.
Scholes, mwenye miaka 35, bado anaendelea kung’ara na juzi huko Milan, Italia alifunga bao moja katika ushindi wa bao 3-2 dhidi ya AC Milan kwenye mechi ya UEFA.
Ferguson amesema Scholes bado ana uwezo mkubwa wa kucheza na wataongea nae ili kurefusha mkataba wake.
Msimu huu Scholes amecheza mechi 25 kati ya 40 za Man United na amefunga bao 5.
Scholes alianza kuichezea Manchester United tangu akiwa mtoto na ameshacheza zaidi ya mechi 600 na kushinda Ubingwa wa Ligi Kuu mara 9 na Ubingwa wa Ulaya mara mbili, mwaka 1999 na 2008.
Ameichezea England mara 65 na kuamua kustaafu mwaka 2004 ili atilie mkazo kuichezea Man United tu.
Wachezaji Chelsea waambiwa: “Shikeni adabu zenu!”
Menejimenti ya Chelsea, hasa Mmiliki, Roman Abramovich, imewataka Wachezaji wa Chelsea kuchunga tabia na mienendo yao ili kujiepusha kuingizwa katika skandali ambazo licha ya kuwachafulia majina yao pia inaharibu jina la Klabu ya Chelsea.
Wito huo umefuatia kashfa ya Nahodha wao John Terry aliehusishwa na kutembea na gelfrendi wa Mchezaji mwenzake Wayne Bridge na skandali hiyo ilimsababisha kuvuliwa Unahodha wa England.
Pia kumekuwa na taarifa zinazomtaja Ashley Cole kukumbwa na kashfa inayotingisha ndoa yake.
Ron Gourlay, Mkurugenzi Mtendaji wa Chelsea, alifanya mkutano na Wachezaji wote wa Klabu hiyo na kuwataka wajichunge au Klabu italazimika kutoa adhabu kali.

No comments:

Powered By Blogger