Ghana 1 Serbia 0
Ghana leo imekuwa Timu ya kwanza toka Afrika kuonja ushindi katika Fainali za Kombe la Dunia huko Uwanja wa Loftus, Pretoria walipoifunga Serbia kwa bao 1-0, bao la penalti ya dakika 85 Mfungaji akiwa Asamoah Gyan.
Timu nyingine za Afrika ambazo tayari zimeshacheza mecho moja moja ni Wenyeji Afrika Kusini waliotoka sare ya 1-1 na Mexico na Nigeria waliofungwa 1-0 na Argentina.
Hadi mapumziko, Serbia na Ghana zilikuwa hazijafungana na matukio yote makuu yalitokea Kipindi cha Pili.
Kwenye dakika ya 74 Serbia walibakia Mtu 10 baada ya Alexander Lukovic kupewa Kadi ya Njano ya pili na hivyo kuwashwa Nyekundu na kutolewa baada ya kumshika Asamoah Gyan aliekuwa anachoropoka.Licha ya kucheza pungufu Serbia bado kidogo wapate bao dakika ya 79 kupitia Krasic lakini Kipa Kingston aliokoa vizuri sana.
Ndipo ilipotimu dakika ya 83 na Ghana kupewa penalti baada ya Beki Kuzmanovic kuunawa mpira wa juu.
Asamoah Gyan akapiga penalti hiyo na kumpeleka mbovu Kipa Stojkoviv na kuipa Ghana bao muhimu na la ushindi.
Katika dakika ya 92, Gyan tena angepata bao la pili lakini bomba yake ikagonga mwamba.
Mechi inayofuata Ghana wataivaa Australia Juni 19 na Serbia watapambana na Ujerumani Juni 18.
Timu:
Serbia: Stojkovic; Ivanovic, Vidic, Lukovic Kolarov; Krasic, Stankovic, Milijas, Jovanovic; Zigic, Pantelic.
Ghana: Kingson; Pantsil, Mensah, Vorsah, Sarpei; Annan, Asamoah, Ayew, Boateng; Asamoah Gyan, Tagoe.
Refa: Hector Baldassi (Argentina)
No comments:
Post a Comment