Wednesday 16 June 2010

TEMBELEA: www.sokainbongo.com

FIFA yatupa ombi la Ufaransa la Kipa mpya
FIFA imeikatalia Ufaransa kumwita Kipa mpya baada ya mmoja wa Makipa wao watatu kuumia juzi Jumatatu na maumivu hayo yatamweka nje kwa Mwezi mmoja.
Kipa Cedric Carrasso, Miaka 28, ameumia musuli pajani na Ufaransa ilitaka kumwita Stephane Ruffier lakini FIFA imegoma na kusema kanuni zinaeleza wazi Timu haziruhusiwi kumbadili Mchezaji baada ya kucheza mechi zao za kwanza.
Kanuni za FIFA za Fainali za Kombe la Dunia zinaruhusu Timu kubadili Mchezaji alieumia mpaka Masaa 24 kabla ya Mechi yao ya kwanza.
Hata hivyo kuumia kwa Carrasso hakutaiathiri sana Ufaransa kwani Kipa Nambari wani ni Hugo Lloris wa Lyon na msaidizi wake ni Steve Mandanda wa Marseille na wote wako fiti.
Maradona ashambulia tena!!
Katika Mkutano na Wanahabari leo Alhamisi Juni 16 huko Afrika Kusini, Kocha wa Argentina Diego Maradona amerudia tena kumshambulia Pele na pia safari hii amemwingiza Rais wa UEFA, Michel Platini, ambae alikuwa Mchezaji Staa wa Ufaransa Miaka ya nyuma.
Hivi majuzi Pele aliripotiwa akijibu shutuma za Maradona za awali kwa kusema Maradona amechukua kazi ya Ukocha wa Argentina kwa vile alikuwa hana kazi na anahitaji pesa.
Maradona sasa amemtaka Pele arudi Makumbusho akimaanisha abaki tu awe kumbukumbu.
Akimgeukia Platini ambae aliwahi kuuhoji uwezo wa Maradona kama Kocha, Maradona alidai: “Platini? Sishangai kuhusu yeye kwani nimekuwa na uhusiano wa ‘habari nzuri na kwa heri tu’ na yeye! Tunajua Wafaransa walivyo na Platini ni Mfaransa na anaamini yeye ni bora kuliko mtu yeyote!”
Kisha Maradona akauvaa Jabulani, mpira rasmi wa Fainali hizi, na akatamka: “Sitaki kuzungumza kuhusu mpira huu kwa sababu kila mtu anauzungumza lakini ni muhimu! Nawataka Pele na Platini waende uwanjani waucheze huu Jabulani na wauangalie kama mzuri au mbaya na waache kuzungumza upuuzi kuhusu mimi!”

No comments:

Powered By Blogger