Tuesday 15 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Beckenbauer aikandya England!
Franz Beckenbauer ameiponda England kwa kucheza ‘butua butua’ na amedai hilo linatokana na kutokuwa na vipaji vya nyumbani kwenye Ligi Kuu na badala yake kutegemea Wageni.
Wakati kwenye Fainali za Kombe la Dunia huo Afrika Kusini Nchi ya Beckenbauer imeanza vizuri kwa kuiwasha Australia 4-0, England imeanza kwa kusuasua kwa kuambua sare ya 1-1 na USA huku Kipa wa England Robert Green akiipa goli la zawadi USA.
Beckenbauer, Miaka 64, alikuwa Kepteni wa Germany iliyonyakua Kombe la Dunia Mwaka 1974.
Mkongwe huyo ametamka: “Niliiona England ikicheza na USA na hio haikuwa Soka na inaelekea wamerudi nyuma Kisoka kwani wanacheza mpira wa kizamani wa kubutua na kukimbiza tu!”
Beckenabauer aliongeza kwa kudai haoni kama Kocha wa England Fabio Capello anaweza kuibadili Timu.
Adidas imewanufaisha Ujerumani kwa Jabulani!!!
Beki wa England, Jamie Carragher, amedai Ujerumani imenufaika sana na kuucheza mpira wa Jabulani kwa muda mrefu kwa vile Watengenezaji wake, Adidas, ni Kampuni ya Kijerumani na vilivile ni Wadhamini wa Bundesliga na hivyo Ligi hiyo ilianza kuutumia mpira huo tangu Msimu uliopita.
Timu nyingi pamoja na Wachezaji wengi sana walio Fainali za Kombe la Dunia wameulaumu mpira huo Jabulani kwamba ni mgumu kuumiliki, kuucheza na pia huwababaisha sana Makipa kwa vile hupinda na kubadilisha mwelekeo ukishapigwa.
Carragher amedai: “Wamenufaika kwa kuutumia muda mrefu kwani mpira huu ni tofauti mno!”
Hata hivyo, Carragher amekiri Ujerumani ilicheza vizuri mno ilipowabamiza Australia 4-0.


Ivory Coast 0 Ureno 0
Huku mvua ikianguka Uwanjani Nelson Mandela Mjini Port Elizabeth, Ivory Coast na Ureno zilitoka sare ya 0-0 kwenye mechi ambayo nafasi zilikuwa adimu sana.
Supastaa Cristiano Ronaldo alikaribia kufunga pale shuti lake lilipogonga mwamba lakini baada ya hapo alifunikwa kabisa.
Ivory Coast walianza mechi hii bila ya Nahodha na Supastaa wao Didier Drogba ambae ndie Mchezaji Bora Afrika na Mfungaji Bora Ligi Kuu England ambae alivunjika mfupa mkononi kwenye mechi ya kirafiki na Japan huko Uswisi takriban siku 10 zilizopita na kulazimika kufanyiwa operesheni.
Ilibidi Drogba aombewe kibali maalum toka FIFA ili acheze mechi hii huku akiwa amevaa gamba gumu mkononi kuulinda na aliingizwa Kipindi cha Pili kuchukua nafasi ya Mchezaji mwenzake wa Chelsea Kalou na nusura afunge goli lakini shuti lake halikulenga
Mechi inayofuata kwa Ivory Coast ni dhidi ya Brazil Juni 20 na Ureno wataikumba Korea Kaskazini Juni 21.
Timu:
Ivory Coast: Barry, Demel, Toure, Zokora, Tiene, Eboue, Toure Yaya, Tiote, Gervinho, Dindane, Kalou.
Portugal: Eduardo, Ferreira, Bruno Alves, Carvalho, Fabio Coentrao, Deco, Mendes, Raul Meireles, Ronaldo, Liedson, Danny.
Refa: Jorge Larrionda (Uruguay)

No comments:

Powered By Blogger