TEMBELEA: www.sokainbongo.com
Spain na Mchawi nani!!!!
Siku moja baada ya kuchapwa 1-0 bila kutegemea na Uswisi kwenye mechi yao ya kwanza ya Kundi H Fainali za Kombe la Dunia, Spain nzima imekuwa ikihaha kutafuta mchawi nani huku Magazeti na Vyombo vingine vya Habari vikilenga lawama zao kwa Timu kwa ujumla, Wachezaji kibinafsi na hata Refa Howard Webb kutoka England aliebebeshwa lawama za kufungwa Mabingwa hao watarajiwa wa Dunia kwa goli walilodai ni ofsaidi.
Gazeti kubwa na maarufu huko Spain na shabiki mkubwa wa Real Madrid, Marca, lilmetamka: "Spain haiwezi tena kuota ndoto ya kuwaza nani mpinzani wao Raundi inayofuata! Sasa ni kujinusuru tu!”
Marca waliendelea kwa kumnukuu Meneja wa zamani wa Spain, Luis Aragones, ambae alisema: “Spain ilicheza bila kujiamini.”
Aragones akaongeza kuwa kufungwa na Uswisi ni pigo kubwa na yeye angekuwa bado Kocha asingetumia Viungo wawili wa kuzuia mipira kama walivyochezeshwa Xabi Alonso na Sergio Busquets kwa pamoja.
Nae Kipa wa Spain Iker Casillas alitoa masikitiko yake kwa kusema wao hawakutegemea kipigo hicho na wamesikitishwa mno.
Beki Gerard Pique akazungumza: “Sasa huu ujinga kuwa sisi ni Mabingwa watarajiwa na kwamba tutatwaa Kombe la Dunia kirahisi tuusahau!”
Lakini Magazeti mengine ya Spain yamemtoa Refa Howard Webb kama mbuzi wa kafara kwa kudai goli la Uswisi lilikuwa ofsaidi na pia Mchezaji wa Uswisi Stephane Grichting alipaswa kuwashwa Kadi Nyekundu kwa kumchezea rafu Andres Iniesta wakati akiwa ndie Beki wa mwisho.
Gazeti la Marca lilizidi kumlaumu Refa Howard Webb kwa vilevile kuinyima Spain penalti kwa madai David Silva alichezewa madhambi.
Gazeti jingine kigogo lilishambulia Timu na baadhi ya Wachezaji kwa kudai Timu ilikuwa ikiremba kupindukia na Mabeki Pique na Puyol ndio wakosaji kwa kuruhusu Uswisi kufunga na kosa hilo wamekuwa wakilifanya mara kwa mara Klabuni kwao FC Barcelona.
Ni Gazeti moja tu lililojaribu kuinua mioyo ya Watu kwa kuandika Bango kubwa: ‘Bado inawezekana!’ pengine wameisahau historia kwamba hakuna hata Timu moja ilitwaa Kombe la Dunia baada ya kufungwa mechi yake ya kwanza kwenye Fainali.
No comments:
Post a Comment