Wednesday 27 May 2009

BIGI MECHI: MANCHESTER UNITED v BARCELONA
Leo, kuanzia saa tatu dakika arobaini na tano usiku bongo taimu, dunia nzima iko ndani ya Roma, Italia kwenye Stadio Olimpico kushuhudia Mabingwa Watetezi ambao pia ndio Mabingwa wa Dunia, Manchester United ya England, wakivaana na Mabingwa wa Spain, Barcelona, kugombea Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya linaloitwa UEFA CHAMPIONS LEAGUE CUP. Ni mechi inayowakutanisha Mameneja wawili wenye tofauti ya miaka 29 kati yao.
Pep Guardiola, Meneja wa Barcelona, ana umri wa miaka 38 na huu ndio msimu wake wa kwanza kuongoza katika soka.
Sir Alex Ferguson, Meneja wa Manchester United, ana miaka 67 na huu ni msimu wake wa 23 akiwa na Man U.
Wakati Pep Guardiola amewahi kulitwaa Kombe hili la Klabu Bingwa Ulaya alipokuwa Mchezaji wa Barcelona mwaka 1992, Sir Alex Ferguson leo anajaribu kulichukua kwa mara ya 3 akiwa kama Meneja wa Manchester United. Ferguson alitwaa Kombe hili mwaka 1999 huko Nou Camp, nyumbani kwa Barcelona, walipowafunga Bayern Munich bao 2-1 na mwaka jana huko Moscow, Urusi walipowabwaga Chelsea.
Ingawa Mameneja hawa wana tofauti kubwa kati yao, kitu kimoja kinachofanana kati yao ni ile falsafa yao ya jinsi ya kusakata soka. Wote ni waumini wa staili ya soka ya pasi za haraka, bila ya kudhoofisha defensi zao na kushambulia kwa haraka.
Ingawa kila Timu imesheheni Mastaa wenye vipaji vya kila aina vinavyosifika na kutambulika dunia nzima, wataalam kadhaa wametoa maoni yao na kubainisha kuwa mechi ya leo itakuwa na mvuto katika sehemu tatu zitakazohusu vita binafsi kati ya Wachezaji wa pande hizo mbili kama ifuatavywo:
-Rio Ferdinand v Samuel Eto'o
Ferdinand ana nguvu, spidi na ni mwepesi kuusoma mchezo na bila shaka atakabiliana vyema na kutakuwa na ushindani mkubwa kati yake na Samuel Eto'o ambae amefunga magoli 35 kwenye La Liga huko Spain.
-Lionel Messi v Patrice Evra
Barcelona sio timu inayotegemea Mchezaji mmoja lakini, bila shaka, Lionel Messi ni mmoja wa Wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu sana duniani. Kawaida, Barcelona humpanga Messi winga ya kulia ili awe anaingia ndani kwa kutumia mguu wake bora wa shoto na kupiga chenga au kubadilishana pasi fupi na wenzake. Itabidi Evra awe makini dakika zote 90 kama alivyofanya kwenye mechi za Nusu Fainali za msimu uliopita alipomudu kumzima Messi na Man U kuibuka washindi.
-Cristiano Ronaldo v Sylvinho
Barcelona wana pengo kubwa kwenye defensi baada ya kufungiwa Mafulubeki wao wote wawili Dani Alvez na Eric Abidal. Hivyo, pengine, itabidi achezeshwe Beki wa zamani wa Arsenal Sylvinho ambae ni wazi sasa jua linamchwea. Itakuwa si ajabu kwa Sir Alex Ferguson kumpanga Cristiano Ronaldo winga ya kushoto ili apate mwanya kwa Beki huyu 'mchovu.'
Vikosi:
Manchester United [Mfumo, pengine, 4-3-3]:
Van der Sar, O'Shea, Ferdinand, Vidic, Evra, Carrick, Giggs, Anderson, Park, Ronaldo, Rooney.
Barcelona [Mfumo, pengine, 4-1-4-1]:
Valdes, Puyol, Pique, Toure, Sylvinho, Busquets, Henry, Xavi, Iniesta, Messi, Eto'o
Refa: Massimo Busacca kutoka Switzerland
NANI KASEMA NINI?
Sir Alex Ferguson: 'Mara nyingi tumeona mechi doro zinazochezwa kwa timu kujihami mno! Soka siku zote linataka liwe la kuvutia. Manchester United na Barcelona wanaweza kucheza soka tamu na la kuvutia!! Kila timu ina wachezaji wenye vipaji sana!! Leo tunacheza na timu bora yenye historia kubwa sana!! Niliwaona ile mechi yao waliyowafunga Real Madrid 6-2 na nikasema 'Mungu wangu!! Tunacheza nao hawa!!' Lakini hawa wanafungika!!'
Pep Gurdiola: 'Hii ni siku muhimu sana katika maisha yangu ya uchezaji na na kama kocha! Tuna staili yetu ya kucheza lakini kuna staili nyingi za uchezaji!! Hivyo hatujioni ni bora! Itabidi tutilie mkazo mbinu zetu tu! Lakini kama tutashindwa kumudu 'miguvu' ya Manchester United basi tutazama!!'
Lionel Messi: 'Kama tukicheza kama tulivyocheza msimu wote basi tuna nafasi! Man U na sisi tunacheza staili moja, wote tunamiliki mpira! Lakini wao ni Mabingwa Watetezi hivyo wako mbele yetu!'
Rio Ferdinand: 'Tukijihami mno kwenye mechi hii ni hatari kwetu kwani wana vipaji vikubwa!! Tuna uwezo mkubwa wa kujilinda na kushambulia!! Ni ngumu kumdhibiti Messi, ni mchezaji mzuri sana lakini tushammudu kabla!!'
Jordi Cruyff [Mtoto wa Johan Cruyff na ambae alichezea timu zote mbili Man U na Barcelona]: 'Ferguson ni mbweha mjanja sana na lazima atawashangaza watu kwa upangaji timu na mfumo wake na kuwafunga Barca!! Nilipokuwa Old Trafford alikuwa akifanya maamuzi ya ajabu na yenye mafanikio makubwa!! Anaweza kumchezesha Mchezaji ambae hategemewi kabisa na kila mara uamuzi huo hufanikiwa!! Ni Mcheza kamari mahiri!!!'
Marcel Desailly: 'Kila Timu ina Wachezaji bora lakini Barca wako mbele kiduchu!! Kama wakiweza kusimama imara kwenye ngome watashinda!!'
Nahodha wa Chelsea, John Terry: 'Naweza kuwasha TV hafutaimu au mwisho wa mchezo kujua matokeo! Sitatizama mechi, ntawaogesha wanangu na kulala mapema!!!'
MWISHONI:
Shabiki aliyekubuhu wa Barcelona: 'MANCHESTER UNITED WANAWEZA KUSHINDA!!! LAKINI NI JUU YA DAMU, JASHO NA MACHOZI YA BARCELONA YOTE!!!'
Sir Alex Ferguson alipoambiwa Manchester United leo wanavaa jezi nyeupe tupu kama Real Madrid ili kuwakera Barcelona alicheka na kusema: 'Tunafurahia jezi hii lakini sisi ni bora sana kuliko Real Madrid!!!'

No comments:

Powered By Blogger