Tuesday, 26 May 2009

Roma yaanza kujidhibiti kwa uvamizi!!!

Masanga marufuku kuanzia Jumanne hadi Alhamisi!!!!


Viongozi wa Jiji la Roma, Italia wameanza kujizatiti kukabiliana na uvamizi wa Washabiki zaidi ya 67,000 wanaotarajiwa kutua mjini humo ili kushuhudia Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya, lijulikanalo rasmi kama UEFA CHAMPIONS LEAGUE, litakalochezwa ndani ya Stadio Olimpico kati ya Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo Manchester United na Barcelona.
Inasadikiwa zaidi ya Mashabiki 30,000 watatoka Uingereza na 20,000 watatoka Spain na ili kukabiliana na vurugu zinazoweza kutokea kati ya pande hizo Viongozi wa Roma wamezuia uuzwaji wa pombe kwa kutumia glasi katika maeneo yanayozunguka Stadio Olimpico kuanzia Jumanne jioni hadi Alhamisi asubuhi na pia usafiri wa sehemu mbalimbali Jijini humo umewekewa vizuizi kadhaa.
Vilevile, uuzwaji wa pombe kwa njia ya 'tekiawei' umepigwa marufuku.
Polisi wametangaza vita maalum kukabiliana na tiketi za bandia kwani inaaminika kuna Mashabiki zaidi ya 5,000 hawana tiketi na watatua Roma ili kubahatisha kupata tiketi dakika za mwisho kitu ambacho kitachochea uhalifu wa tiketi za bandia.
Hadi sasa Polisi wamethibitisha kukamata lundo la tiketi feki. Mkuu wa Polisi wa Roma Giuseppe Pecoraro amethibitisha: 'Tiketi zimekwisha! Zilizobaki zinazouzwa ni feki!!'
Na ili kudhibiti usalama, Polisi wa Italia watasaidiwa na Maafisa kadhaa wa vyeo vya juu kutoka England na Spain.
Mourinho aula zaidi inter Milan!!!
Jose Mourinho ameongezewa mkataba hadi mwaka 2012 na Klabu yake ya Inter Milan mara tu baada ya kuiwezesha Klabu hiyo ya Serie A Italia kutwaa Ubingwa wa Italia kwa mara ya 4 mfululizo.
Huu ni msimu wake wa kwanza kwenye Klabu hiyo.
Mourinho, ambae kabla ya kwenda Inter Milan alikuwa Meneja wa Chelsea, atamaliza mkataba wake tarehe 30 Juni 2012.
Hatua hii imezima ule mvumi mkubwa kuwa Mourinho ataenda Real Madrid msimu ujao.
Sunderland yagoma kumsajili Cisse kwa mkataba wa kudumu!!
Klabu ya Sunderland, ambayo juzi ilikuwa chupuchupu kuteremshwa Daraja, imetangaza kuwa Mshambuliaji toka Ufaransa, Djibril Cisse, hatopewa mkataba wa kudumu Klabuni hapo.
Cisse alijiunga Sunderland kwa mkopo kutoka Klabu ya Marseille ya Ufaransa huku kukiwa na kipengele kwenye mkopo huo kuwa Sunderland inaweza kumsaini kwa mkataba wa kudumu endapo itaafiki.
Lakini, Mwenyekiti wa Sunderland, Niall Quinn, ametangaza kupitia tovuti ya Klabu hiyo kuwa hawatomchukua Cisse ambae msimu huu alichezea Klabu hiyo mechi 38 na kuifungia mabao 11.
Gordon Strachan atimka Celtic!!!
Meneja wa Celtic, Gordon Strachan, amejiuzulu mara tu baada ya kuutema Ubingwa wa Scotland hapo juzi baada ya Mahasimu wao wakubwa Rangers kuutwaa Ubingwa huo.
Strachan aliiongoza Celtic kutwaa Ubingwa wa Scotland kwa misimu mitatu iliyopita.
Viera arudi kundini Ufaransa!!!
Kiungo veterani wa Ufaransa, Patrick Vieira [32], anaechezea Klabu Bingwa ya Italia Inter Milan, amerudishwa tena kwenye Timu ya Taifa ya Ufaransa na Kocha Raymond Domenech baada ya kukosa mechi 15 zilizopita za Ufaransa kwa kuwa majeruhi.
Ufaransa inategemewa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Nigeria hapo Juni 2 na siku tatu baadae watacheza na Uturuki.
Kikosi kamili cha Ufaransa na Klabu wanazotoka:
Makipa: Cedric Carrasso (Toulouse), Hugo Lloris (Olympique Lyon), Steve Mandanda (Olympique Marseille).
Walinzi: Eric Abidal (Barcelona), Jean-Alain Boumsong (Olympique Lyon), Patrice Evra (Manchester United), Rod Fanni (Stade Rennes), Philippe Mexes (AS Roma), Bacary Sagna (Arsenal), Sebastien Squillaci (Sevilla), Julien Escude (Sevilla).
Viungo: Patrick Vieira (Inter Milan), Abou Diaby (Arsenal), Alou Diarra (Girondins Bordeaux), Lassana Diarra (Real Madrid), Yoann Gourcuff (Girondins Bordeaux), Jeremy Toulalan (Olympique Lyon), Florent Malouda (Chelsea).
Washambuliaji: Nicolas Anelka (Chelsea), Karim Benzema (Olympique Lyon), Andre-Pierre Gignac (Toulouse), Thierry Henry (Barcelona), Franck Ribery (Bayern Munich), Sidney Govou (Olympique Lyon), Loic Remy (Nice)

No comments:

Powered By Blogger