Tuesday 26 May 2009

KITIMTIM ROMA KESHO!!!
Manchester United v Barcelona Stadio Olimpico Saa 3 dak 45 usiku Bongo Taimu
Kesho ndio kimbembe cha mwisho cha Klabu Bingwa Ulaya wakati Mabingwa Watetezi Manchester United watakapoingia Uwanjani Olimpico huko Roma, Italia kutetea taji lao kwa kupambana na Timu ngumu ya Barcleona katika Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Hii ni mara ya 10 kwa Klabu hizi kukutana katika Mashindano mbalimbali ya Klabu za Ulaya huku Manchester United akiongoza kwa kushinda mechi 3, Barcelona ameshinda mara 2 na mechi 4 ziliisha droo. Klabu hizi zimewahi kukutana kwenye Fainali ya mwaka 1991 ya Kombe la Mabingwa wa Kikombe cha Nchi [European Cup Winners Cup] na Manchester United aliibuka mshindi kwa bao 2-1.
Msimu uliokwisha, kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Barcelona alitoka suluhu 0-0 kwake Nou Camp na Manchester United na marudiano yaliyofanyika Old Trafford, nyumbani kwa Manchester United, wenyeji waliibuka washindi kwa bao moja alilofunga Paul Scholes na Manchester United akatinga Fainali na kumtoa Chelsea.
==Safari ya kwenda Roma: Manchester United FC
Manchester United walianzia KUNDI E na walishinda mechi 2 katika mechi 6 za Kundi hili na kumaliza wakiwa vinara. Man U walitoka suluhu mbili na Villareal na kuwafunga Aalborg BK bao 3-0 na Celtic kwa idadi hiyo hiyo.
Katika Raundi ya Kwanza ya Mtoano, Man U walitoka suluhu 0-0 na Timu ya Jose Mourinho, Inter Milan, katika mechi ya kwanza huko Italia na kushinda 2-0 kwenye marudiano Old Trafford.
Kwenye Robo Fainali, Man U walikutana na FC Porto ya Ureno na mechi ya kwanza ndani ya Old Trafford mechi ilikwisha 2-2. Lakini katika mechi ya marudiano huko Ureno, Mreno Cristiano Ronaldo aliwatungua Wareno wenzake kwa kigongo cha mita 35 na kuiingiza Man U Nusu Fainali.
Nusu Fainali ilikuwa ni mechi kati ya Timu mbili toka England, yaani Manchester United v Arsenal, na mechi ya kwanza, iliyochezwa Old Trafford, Manchester United walishinda bao 1-0 kwa goli la Beki John O’Shea.
Marudiano huko nyumbani kwa Arsenal, Emirates Stadium, Manchester United waliibuka kidedea kwa ushindi mtamu wa mabao 3-1 kwa mabao yaliyofungwa na Ji-Sung Park bao moja na Ronaldo mabao mawili.
==Safari ya kwenda Roma: FC Barcelona
Barcelona walikuwa KUNDI C na walianza mechi zao kwa makeke makubwa kwa kuzikung’uta Sporting Clube de Portugal mabao 3-1, FC Basel ya Uswisi mabao 5-0 na pia kwenye mechi ya marudiano wakaibamiza Sporting Clube de Portugal mabao 5-2 huko huko kwao Lisbon, Ureno. Huku wakishajijua wamemaliza Kundi lao kama vinara, Barca walifungwa 3-2 na FC Shakhtar Donetsk.
Katika Raundi ya Kwanza ya Mtoano, Barca walitoka suluhu 1-1 na Olympique Lyonnais, maarufu kama Lyon, huko Ufaransa na marudiano huko Nou Camp waliichabanga Lyon mabao 5-2.
Robo Fainali, Barca walikutana na Wakongwe wa Ujerumani Bayern Munich na kuibamiza 4-0 ndani ya Nou Camp na marudiano huko Ujerumani yalikuwa 1-1.
Kwenye Nusu Fainali, Barca walipambana na Chelsea ya England.
Mechi ya kwanza huko Nou Camp ilikuwa 0-0 na mechi ya pili ikahamia Stamford Bridge, London nyumbani kwa Chelsea na huko ndiko ikazuka VITA KUU YA DARAJANI.
Huku wakiongoza kwa bao moja, bao tamu alilofunga Michael Essien, na licha ya Refa kutoka Norway Tom Henning Ovrebo kuwanyima Chelsea penalti kadha wa kadha za dhahiri, huku Uwanja mzima wa Stamford Bridge wakiamini Chelsea watatinga Fainali, katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza wa majeruhi Iniesta aliachia shuti lililomshinda Kipa Petr Cech na kutinga wavuni kuifanya mechi imalizike 1-1 na Barcelona kuingia Fainali kwa goli la ugenini.

Ndipo kasheshe la kina Drogba na wenzake likaanza na sasa wako kizimbani kwenye Mahakama za UEFA!!!!!
BAADA YA KWISHA LIGI KUU ENGLAND, ZIJUE KLABU ZITAKAZOCHEZA ULAYA MSIMU UJAO 2009/10
Kwa kumaliza nafasi nne za juu Klabu za Manchester United, Liverpool, Chelsea na Arsenal zitaiwakilisha England katika UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu ujao wa 2009/10.
Manchester United, Liverpool na Chelsea zitaingia moja kwa moja kwenye hatua ya MAKUNDI ambayo inachezwa kwa mtindo wa Ligi wa mechi za nyumbani na ugenini.
Arsenal, kwa kumaliza nafasi ya 4 kwenye LIGI KUU, atacheza UEFA CHAMPIONS LEAGUE kwenye hatua ya awali ya Mtoano na anaweza kupangiwa Klabu ya Nchi yeyote ile bila kubagua Nchi kubwa au Klabu kubwa kama ilivyokuwa zamani ambapo Timu kubwa zilikuwa zikitenganishwa kwenye awamu hii.
Klabu zilizomaliza nafasi ya 5 hadi ya 7 msimu ujao zitacheza kwenye mashindano mapya yatakayojulikana kama UEFA EUROPA LEAGUE. Mshindano haya yalikuwa yakiitwa UEFA CUP na msimu ujao mfumo wake utafanana na UEFA CHAMPIONS LEAGUE kwani Klabu zitapangwa kwenye Makundi na kucheza mtindo wa Ligi kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Timu zitakazowakilisha England kwenye UEFA EUROPA LEAGUE ni Everton, Aston Villa na Fulham.
ZAWADI ZA KILA TIMU ZA LIGI KUU ENGLAND ZATANGAZWA!!!
Wasimamizi wa LIGI KUU England wametangaza zawadi ya kitita babu kubwa ambazo kila Klabu itaopoa kufuatana na nafasi iliyoshika kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
Mbali ya zawadi hiyo ya Bulungutu kubwa, kila Klabu itapewa Pauni Milioni 23.6 ikiwa ni haki yao ya maonyesho ya mechi kwenye TV na pia nyongeza ya Pauni Milioni 5 kwa kila Klabu pamoja na kitita kingine ambacho kitategemea Klabu ilionyeshwa laivu mara ngapi.
Zawadi zinazotokana na Msimamo wa Ligi ni kama ifuatavywo [Fedha ni Pauni za Uingereza na ni Milioni]:
-1. Man U: 15.2
-2. Liverpool: 14.5
-3. Chelsea: 13.7
-4. Arsenal: 12.9
-5. Everton: 12.2
-6. Aston Villa: 11.4
-7. Fulham: 10.7
-8. Tottenham: 9.9
-9. West Ham: 9.1
-10. Man City: 8.4
-11. Wigan: 7.6
-12. Stoke: 6.9
-13. Bolton: 6.1
-14. Portsmouth 5.3
-15. Blackburn 4.6
-16. Sunderland 3.8
-17. Hull 3
-18. Newcastle 2.3
-19. Middlesbrough 1.5
-20. West Brom 0.8

No comments:

Powered By Blogger