Saturday 30 May 2009

Makelele atoboa: ‘Ugomvi kati ya John Terry na Mourinho ulisababisha Mourinho atimuliwe Chelsea!!!’
Kiungo wa zamani wa Chelsea, Claude Makelele [36], amepasua kwenye Kitabu cha Maisha yake kilichochapishwa wiki hii na kuanza kuuzwa leo huko Ufaransa kuwa ugomvi kati ya aliekuwa Meneja wa Chelsea Jose Mourinho na Nahodha wa Chelsea, John Terry, ndio ulisababisha Mmiliki wa Chelsea, Mrusi Roman Abramovich amtimue Mourinho Septemba, 2007.
Claude Makelele, ambae alizaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuhamia Ufaransa mwaka 1977, alikuwa pia Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, ameandika kwenye Kitabu chake kiitwacho ‘Tout Simplement’ kuwa baada ya John Terry kuwa anaumia mara kwa mara Jose Mourinho akaamua kumpumzisha kucheza na ndipo ugomvi mkubwa ukazuka kati yao.
Klabu ya Chelsea pamoja na John Terry mwenyewe wamekanusha taarifa hizo za kwenye Kitabu cha Claude Makelele kwa madai kuwa ukweli umepotoshwa.
Makelele anazungumzia kwenye Kitabu kwa kusema: ‘Nilipata habari za Mourinho kutoka kwa Drogba. Aliniambia kesho atafukuzwa! Nilishangaa sana! Nilidhani Mourinho hagusiki! Siku ya pili tukiwa Cobham, kwenye Uwanja wetu wa mazoezi, ilikuwa ni vurugu! Mapaparazi walijaa kila kona na hata helikopta zilikuwa zinaruka juu ya vichwa vyetu!’
Makelele anaendelea kwenye kitabu chake: ‘Wachezaji wengi walikuwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na nikakutana na Rui Faria, alikuwa ni Mkufunzi wetu wa Mazoezi ya Viungo nikamuuliza kuna nini? Akanijibu Kocha kafukuzwa! Nikamuuliza kwa nni na akasema Wachezaji wengi, akiwemo Terry, wamelalamika kwa Mmiliki kuhusu Mourinho!’
‘Ndio nikagundua, Mourinho alimwambia Terry.....’Makelele anaandika kitabuni. ‘......atabaki benchi kwa mechi kadhaa ili apone vizuri mgongo aliofanyiwa operesheni msimu uliopita kwani tangu wakati huo umekuwa ukimsumbua mara kwa mara. Terry akabisha na kusema yuko fiti. Mourinho akagoma kumchezesha na kumwambia kuanzia siku hiyo Walinzi wa Kati wa Chelsea watakuwa Ricardo Carvalho na Alex! Hapo ndipo ilipotangazwa vita rasmi!’
Makelele anaendelea: ‘Kwa Terry huo ulikuwa usaliti!! Msimu uliokwisha alichezea Klabu huku akiwa na maumivu makali! Terry alitegemea Mourinho angemwona anastahili kila nafasi ya kucheza kwa ushujaa wake. Mourinho alikuwa amechokoza vita mbaya sana! Ingekuwa Mchezaji wenyewe ni mimi au Ballack au Shevchenko hayo yangeisha!! Lakini ni Terry na huyo humgusi Chelsea!’
‘Terry akaenda kwa Mkurugenzi Mtendaji Peter Kenyon na kuomba uhamisho!.’ Makelele amezidi kuelezea kitabuni. ‘Abramovich akashtuka na kuchukua hatua haraka! Alijua Mashabiki na Wachezaji hawawezi kukubali John Terry aondoke! Badala yake Mourinho akaambiwa afungashe virago vyake!!!’
Jose Mourinho aliajiriwa Chelsea Juni 2004 na kufukuzwa tarehe 20 Septemba 2007. Katika kipindi hicho alichokuwa Chelsea aliweza kuchukua Ubingwa wa LIGI KUU England mara 2, Vikombe vya Carling mara 2 na FA Cup moja. Kwa sasa Mourinho ni Meneja wa Inter Milan kwa msimu mmoja sasa na juzi tu amefanikiwa kutwaa Ubingwa wa SERIE A ya Italia.
Kwa sasa Claude Makelele ni Mchezaji wa Klabu ya Ufaransa Paris St Germain.

No comments:

Powered By Blogger