‘Babu’ Sol Campbell arudi Arsenal!!!!
Sol Campbell, miaka 35, yuko katika hatua za mwisho za kurudi kuichezea tena Arsenal baada ya kukichezea Kikosi cha Akiba cha Arsenal kwa dakika 45 hapo jana kilipocheza na Kikosi cha Akiba cha West Ham.
Campbell aliichezea Arsenal kwa mara ya mwisho mwaka 2006 katika Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na kisha akahamia Portsmouth.
Alipotoka Portsmouth alikwenda Notts County lakini huko kukatokea mtafaruku na akajiondoa bila kucheza mechi hata moja na sasa ni Mchezaji huru.
Mwenyewe Campbell amesema ameshasaini Arsenal ila kumebakia kukamilisha taratibu chache na Mkataba wake utamweka hapo mpaka mwishoni mwa msimu.
Campbell amesema Arsene Wenger alimruhusu kufanya mazoezi na Arsenal kwa miezi miwili sasa na baada ya kumchunguza aliridhika kiwango bado kipo cha kucheza Arsenal na ndio maana amepewa mkataba.
KOMBE LA AFRIKA:
Leo Kundi D ni Cameroun v Gabon na Zambia v Tunisia!!
Leo saa moja usiku katika Uwanja wa Taifa wa Tundavala huko Lubango, Angola, Cameroun, moja wa Vigogo wa Afrika, watashuka dimbani kuivaa Gabon katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Cameroun, wakiongozwa na Supastaa wao Samuel Eto’o anaecheza huko Italia Klabu ya Inter Milan, ndio wanategemewa kuibuka kidedea lakini Gabon wana Wachezaji wazoefu kama vile Straika Daniel Cousin anaecheza Ligi Kuu England na Klabu ya Hull City.
Mara baada ya mechi ya Cameroun v Gabon, hapo hapo Uwanjani Tundavala, saa 3 na nusu usiku, saa za bongo, Zambia watapambana na Tunisia.
Mechi hii inategemewa kuwa ngumu kama alivyokiri Kocha wa Tunisia Faouzi Benzarti na kuungwa mkono na Nahodha wa Zambia Christopher Katongo.
Matokeo jana: Mozambique 2-2 Benin
Jana usiku, katika mechi ya pili ya Kundi C ya kugombea Kombe la Mataifa ya Afrika, Benin waliumwaga mchezo huo baada ya kuongoza 2-0 kwa mabao ya Razak Omotoyossi anaechezea FC Metz ya Ufaransa aliefunga kwa penalti dakika ya 15 na Msumbiji kujifunga wenyewe kupitia Dario Khan.
Lakini Msumbiji walijitutumua na kusawazisha kupitia mabao ya Lobo na Goncalves na kuifanya mechi iishe sare ya 2-2.
Katika mechi ya awali ya Kundi hili C, Misri ambao ndio mabingwa Watetezi, waliibwaga Nigeria 3-1.
Mechi zinazofuata kwenye Kundi hili ni Januari 16 wakati Msumbiji watakapocheza na Mabingwa Watetezi Misri na Benini kukutana na Nigeria.
KOMBE LA FA: Coventry 1 Portsmouth 2
Aaron Mokoena, Mchezaji kutoka Afrika Kusini, alifunga bao sekunde za mwisho za muda wa nyongeza na kuipa ushindi wa 2-1 Portsmouth dhidi ya Coventry katika mechi ya marudiano ya Kombe la FA hapo jana.
Leon Best aliipa Coventry bao la kuongoza lakini katika dakika ya 90, Nahodha wa Coventry Stephen Wright alijifunga mwenyewe na kuwapa sare ya 1-1 Portsmouth na hivyo mechi kuingia nusu saa ya nyongeza.
Timu hizi zilitoka sare katika mechi ya kwanza iliyochezwa Fratton Park nyumbani kwa Portsmouth na bao la Mokena limeiingiza Timu hiyo Raundi ya 4 ya FA Cup na itakutana na Sunderland.
Leo saa 4 dakika 45 usiku, saa za bongo, Liverpool watarudiana na Reading katika mechi ya Raundi ya 3 ya Kombe la FA baada ya kutoka sare katika mechi ya kwanza na mechi hii ipo nyumbani kwa Liverpool Uwanjani Anfield.
Mshindi ataingia Raundi ya 4 na atacheza na Burnley.
No comments:
Post a Comment