Monday 11 January 2010

Malawi 3 Algeria 0
Malawi leo huko Luanda, Angola iliistua Afrika na Dunia nzima pale ilipoifumua Timu ya kutegemewa Algeria mabao 3-0 katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Malawi walipata bao lao la kwanza dakika ya 17 kupitia Russel Mwafulirwa na Elvis Kafoteka akaongeza la pili na kuifanya Malawi iwe mbele 2-0 hadi mapumziko.
David Banda akapachika bao la 3 kipindi cha pili dakika ya 50 ya mchezo.
Kipigo hicho cha Algeria, Timu ambayo ndiyo iliwabwaga Misri, Mabingwa wa Afrika, nje ya Kombe la Dunia na kuwaingiza wao Fainali za Kombe la Dunia, ni maajabu kwa wengi.
Katika mechi zijazo za Kundi hili Angola watacheza na Malawi na Algeria watapambana na Mali mechi ambazo zitachezwa Januari 14.
Mkurugenzi Liverpool ajiuzulu baada ya kumtusi Shabiki!!!
• Ni Mtoto wa Mmiliki wa Liverpool Tom Hicks!!
Chama cha Washabiki wa Liverpool kiitwacho ‘Spirit of Shankly’ kimetoa shinikizo kubwa na kusababisha Mtoto wa mmoja wa Wamiliki wa Klabu hiyo Tom Hicks ambae pia jina lake ni Tom Hicks, Junior, miaka 39, na ambae ni Mkurugenzi wa Bodi ya Liverpool, kujiuzulu baada ya kumtumia Shabiki mmoja wa Liverpool barua pepe yenye matusi ikiwa ni majibu kwa Shabiki huyo aliehoji Madeni na hatima ya Timu yao kufuatia kutofanya vizuri uwanjani.
Barua pepe hiyo ilimwita Shabiki huyo ‘mpumbavu’ na kuandamana na matusi na kumalizia na kauli ‘nenda jehanamu, unanitia kichefuchefu!’
Ndipo Chama cha Mashabiki wa Liverpool walipomtaka Mkurugenzi huyo Tom Hicks, Junior, kuchukua ‘njia ya kiungwana na kujiuzulu’.
Liverpool inamilikiwa na Baba yake Tom Hicks Junior, aitwae Tom Hicks ambae ni Mmarekani, pamoja na Mmmarekani mwenzake aitwae David Gillett na Wamarekani wote hao wawili wanapingwa vikali na Kundi hilo la Mashabiki ‘Spirit of Shankly’ lenye dhamira ya kuwang’oa.
Jina la Kundi hilo la Mashabiki linatokana na Bill Shankly aliekuwa Meneja shupavu wa Liverpool miaka ya 80 alieleta mafanikio makubwa kwa Klabu hiyo kwa kuiwezesha kutwaa Mataji mengi ya Ubingwa wa England na Ulaya.
Man U yatangaza faida!!!
Manchester United wametangaza faida kwa Mwaka wa Fedha ulioisha Juni 20, 2009 ya Pauni Milioni 48 na pia wametaja mipango yao ya kuzalisha Pauni Milioni 500 kwa kuuza Hati za Dhamana za Klabu hiyo yenye mvuto mkubwa Duniani kote.
Faida hiyo imepigwa jeki hasa kwa mauzo ya Mchezaji Cristiano Ronaldo kwa Real Madrid ya Spain waliemnunua kwa zaidi ya Pauni Milioni 80 mwaka jana.
Wakati huo huo, Manchester United imethibitisha kuwa Msimu ujao Kampuni kubwa ya Kifedha huko Marekani, Aon, ndio watakuwa Wadhamini wa Jezi badala ya AIG na jina la AON ndilo litakuwa kifuani mwa Jezi za Man U.

No comments:

Powered By Blogger