LIGI KUU: TATHMINI YA MECHI ZA WIKIENDI HII
Wikiendi hii inategemewa Timu zote 20 za Ligi Kuu zitashuka dimbani na kucheza tofauti na wikiendi iliyopita wakati mechi zote ziliahirishwa kwa sababu ya barafu na baridi kali isipokuwa mechi mbili tu.
RATIBA:
[saa za bongo]
Jumamosi,
[saa 9 dak 45 mchana]
Stoke v Liverpool
[saa 12 jioni]
Chelsea v Sunderland
Man United v Burnley
Portsmouth v Birmingham
Tottenham v Hull City
Wolves v Wigan
[saa 2 na nusu usiku]
Everton v Man City
Jumapili,
[saa 10 na nusu jioni]
Aston Villa v West Ham
[saa 12 jioni]
Blackburn v Fulham
[saa 1 usiku]
Bolton v Arsenal
Uhondo huu utaanza kwa mechi ya Jumamosi ya mapema kupita zote, ile ya saa 9 dakika 45 mchana, saa za bongo, Stoke City itakapoikaribisha Liverpool.
Baada ya kutolewa nje ya Kombe la FA hapo juzi walipofungwa 2-1 na Reading, Meneja wa Liverpool Rafa Benitez amewaahidi Washabiki wao kuwa katika mechi hii watabadilika na kuwaletea faraja.
Lakini mbali ya Stoke City kuwa wagumu wakiwa nyumbani kwao, Liverpool watakuwa na upungufu mkubwa kwani watawakosa Nyota wao Fernando Torres, Steven Gerard na Yossi Benayoun ambao ni majeruhi.
Vinara Chelsea watakuwa nyumbani Stamford Bridge kucheza na Sunderland na hii ni mechi ya kwanza kwa Chelsea bila ya Mastaa Didier Drogba, Michael Essien na Salomon Kalou ambao wako Angola na Nchi zao kwa Kombe la Afrika.
Burnley, baada ya kuondokewa na Meneja wao Owen Coyle aliehamia Bolton, watakuwa chini ya Meneja mpya Brian Laws huko Old Trafford kucheza na Mabingwa Watetezi Manchester United ambao waliikimbia barafu ya Uingereza wiki yote hii na kujichimbia Doha, Qatar kwa kambi ya mazoezi. Katika mzunguko wa kwanza, Burnley iliipiga Man U bao 1-0.
Portsmouth, Timu iliyo mkiani Ligi Kuu na yenye uhaba mkubwa wa fedha hadi Wachezaji kukosa Mishahara kwa wakati, watakuwa nyumbani kuwakaribisha Birmingham, Timu ambayo kwa sasa ina maendeleo mazuri mno Ligi Kuu. Mechi iliyopita Birmingham ilitoka sare 1-1 na Man U.
Hull City walio nafasi ya pili toka mkiani wanasafiri hadi White Hart Lane kukumbana na Tottenham.
Uwanjani Molineux, Wolves watakuwa wenyeji wa Wigan na Timu zote hizi ziko nafasi ya chini kwenye msimamo wa Ligi hivyo hii ni vita kuu kati yao.
Mechi ya mwisho Jumamosi itakayoanza saa 2 na nusu usiku saa za bongo ni ile ya Goodison Park kati ya wenye uwanja Everton na Manchester City na mechi hii Wadau wanasema ndio mtihani mkubwa kwa Meneja wa Man City Roberto Mancini tangu aanze kazi.
Jumapili, Aston Villa wanawakaibisha West Ham na Villa watapigana washinde mechi hii hasa baada ya kupoteza mechi mbili za mwisho za Ligi. Kwa West ham, Msimu huu ni mgumu sana kwao na Meneja wao Gianfranco Zola ataomba Timu yake ijitutumue.
Mechi nyingine za Jumapili ni Blackburn Rovers v Fulham na Bolton v Arsenal.
Kwa Bolton, hii ni mechi ya kwanza chini ya Meneja mpya Owen Coyle aliehamia hapo kutoka Burnley.
No comments:
Post a Comment