LIGI KUU England: Arsenal na Man U chupuchupu jana!!!!!
• Nini Wenger na Fergie wamesema baada ya sare zao?
Katika mechi mbili pekee za Ligi Kuu zilizochezwa jana, huku nyingine 7 kuahirishwa, Timu za Manchester United na Arsenal, ambazo ziko nafasi ya pili na ya tatu, zote ziliponea chupuchupu kufungwa na zote kulazimisha sare na hivyo kushindwa kuwakaribia vinara Chelsea ambao mechi yao na Hull haikuchezwa kwa ajili ya barafu.
Mpaka sasa Chelsea yuko juu akiwa amecheza mechi 20 na pointi 45 mkononi, Man U ni wa pili mechi 21 na pointi 44 na Arsenal ni watatu kwa mechi 20 na pointi 42.
Arsene Wenger wa Arsenal, ambayo Timu yake ilitoka nyuma mara mbili na kuambua suluhu ya 2-2 na Everton, alikiri Everton iliwazidi kila kitu na walibahatika kupata pointi moja.
Wenger alisema: “Walituzuia tusitandaze soka letu la kawaida! Walipokuwa mbele 2-1 nusura wapate la 3 lakini ni bahati na sisi hatukukata tamaa na tukarudisha ikawa 2-2!”
David Moyes wa Everton alisikitishwa na Timu yake kupoteza pointi 3 walipowaruhusu Arsenal kusawazisha dakika za majeruhi na hasa alikiri hawakuwa na bahati kwani goli mbili zote za Arsenal zilitokana na mikwaju iliyowababatiza Mabeki wake na kumhadaa Kipa wake Tim Howard.
Nae Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, licha ya kumsifia Meneja wa Birmigham Alex McLeish, ambae aliwahi kuwa Mchezaji wake wakati yeye ni Kocha wa Aberdeen ya Scotland, kwa kuisuka vyema Birmingham na kuifanya haijafungwa katika mechi 12 mfululizo za Ligi Kuu, pia alimlaumu Mwamuzi Mark Clattenburg.
Ingawa Manchester United walitawala kipindi chote cha kwanza, ni Birmingham ndio walifunga bao dakika ya 39 kupitia Cameron Jerome na Man U wakasawazisha dakika ya 63 kwa goli la kujifunga wenyewe baada ya krosi ya Evra kuingizwa wavuni na Beki wa Birmingham Scott Dann.
Lakini Mshika Kibendera alilikataa bao hilo kwa kuashiria Rooney yupo ofsaidi na ndipo yakaanza majadiliano kati ya Refa Clattenburg na Mshika Kibendera huyo kisha Refa Clattenburg akampiku Msaidizi wake na kuamua ni goli.
Katika mechi hiyo, Refa Clattenburg alimtwanga Darren Fletcher wa Man U Kadi mbili za Njano na hivyo kumtoa nje kwa Kadi Nyekundu na kuwaacha wengi wakiishangaa ile Kadi ya pili ya Njano ambayo haikustahili.
Ferguson alizungumzia maamuzi ya Waamuzi wa mechi hiyo: “Sijawahi kuona Mchezaji anatolewa nje kwa rafu ya aina ile! Ni upuuzi mkubwa! Nimekuwa nikimtazama Refa Clattenburg msimu huu na alichezesha mechi ya Arsenal v Tottenham ambayo pengine ilihitajika mtu amtwange mwenzake na shoka ndipo Clattenburg atoe Kadi lakini mechi yetu anamtoa mtu kwa kitu kidogo na cha ajabu!”
Ferguson akaongeza: “Kulikuwa na maamuzi ya ajabu mle! Mshika Kibendera anatoa ofsaidi kwa goli la kujifunga wenyewe! Uliona wapi goli la kujifunga mwenyewe lina ofsaidi?”
Hata hivyo Ferguson amesema wanashkuru kuambulia pointi moja kwani Birmingham chini ya Mchezaji wake wa zamani Alex McLeish ni kiboko.
Katika mechi hiyo ya jana, Sir Alex Ferguson aliweka rekodi mpya kwa kubadilisha Timu katika kila mechi katika mechi 100 mfululizo walizocheza mpaka jana na kufanya katika kila mechi hizo 100 kinashuka Kikosi cha Wachezaji tofauti.
Pengine ubadilishaji huo unaonyesha Man U ina Wachezaji wengi lakini Wadau wengi wanalalamikia hilo linadidimiza uchezaji wa Timu kwani Wachezaji wanakuwa hawachezi kitimu kwani hawaelewani vizuri.
No comments:
Post a Comment