Friday 15 January 2010

KISANGA CHA LIVERPOOL: Ligi Kuu valuvalu, FA Cup…Nje , Carling Cup…Nje, Ubingwa UEFA…Nje, na je Benitez…..NJE??
• Mwenyewe Benitez aomba radhi Mashabiki!!!
Huku kukiwa na kitendawili kikubwa kuhusu ajira yake hapo Liverpool, Meneja Rafa Benitez amewaomba radhi Mashabiki wa Liverpool kwa Timu yake kutofanya vizuri kwenye mechi na mashindano mbalimbali Msimu huu.
Siku ya Jumatano, Liverpool wakiwa nyumbani Uwanjani Anfield, walibwagwa nje ya Kombe la FA baada ya kufungwa na Reading, Timu inayojikongoja Daraja la chini ya Ligi Kuu, kwa bao 2-1.
Benitez, akisoma kutoka kwenye kikaratasi, alisema: “Hatuchezi vizuri na kila mtu kwenye Kikosi chetu anawaonea imani Mashabiki wetu! Kwenye Soka vitu hubadilika haraka na tuamini Jumamosi tutakapocheza na Stoke tutashinda!”
Msimu uliokwisha Liverpool walimaliza nafasi ya pili nyuma ya Mabingwa Manchester United na wakati kila mtu alitegemea watakuwa tishio Msimu huu, mambo yameenda kombo na wamekuwa wakifungwa mechi nyingi na kutupwa nje ya Makombe makubwa.
Kwenye Ligi wako nafasi ya 7 wakiwa pointi 12 nyuma ya vinara Chelsea.
Mpaka sasa wameshatolewa kwenye Vikombe vya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, FA na Carling.
Wamebaki kwenye kinyang’anyiro cha EUROPA Ligi tu na walitupwa huko baada ya kumaliza nafasi ya 3 kwenye Kundi lao la UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Wadau wengi wa Liverpool, wakiongozwa na Wachezaji wa zamani wa Klabu hiyo, wametaka aondolewe lakini hilo kwa uongozi wa Liverpool limekuwa zito ikizingatiwa Klabu hiyo iko kwenye hali mbaya kifedha na inakabiliwa na madeni makubwa.
Kumtimua Benitez ni kuiingiza Klabu hiyo kwenye deni kwani Benitez amesaini Mkataba mpya na Klabu hiyo mwezi Machi 2009 utakaomweka hapo 2014 na ukimtimua tu inabidi umlipe pesa nyingi.
Swali linakuja: Timu ikiendelea kufungwa na hata mwishoye kuikosa nafasi ya kucheza UEFA CHAMPIONS LEAGUE Msimu ujao, nini hatima ya Benitez?
Fergie: 'Rooney atawika Kombe la Dunia'
Sir Alex Ferguson anaamini Wayne Rooney ana uwezo wa kuwa nyota kwenye Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Afrika Kusini mwezi Juni.
Wayne Rooney, miaka 24, alianza kuchezea michuano mikubwa ya Kimataifa pale alipoichezea England kwenye Euro 2004 na kufunga bao 4 lakini akashindwa kuendelea kucheza Mashindano hayo baada ya kuvunjika mfupa kwenye kidole cha mguu wake kwenye Robo fainali walipocheza na Ureno.
Mwaka 2006, huku akitoka kwenye majeruhi, aliichezea England kwenye Kombe la Dunia lakini akatwangwa Kadi Nyekundu kwenye Robo Fainali walipocheza na Ureno.
Lakini Ferguson anasema: “Rooney ana uwezo wa kuwa shujaa wa Kombe la Dunia. Miaka yote kila Kombe la Dunia anaibuka Staa na Rooney ana uwezo huo. Nimeshuhudia jinsi anavyozidi kuboreka!”
Msimu huu, baada ya kuondoka kwa Ronaldo, Rooney ndie amekuwa Mfungaji mkuu wa Manchester United akiwa ni mmoja wa Wafungaji bora wa Ligi Kuu akiwa na bao 14.
Lakini Ferguson anakiri pengo la Ronaldo.
Ferguson anasema: “Ni kweli tunamkosa! Alikuwa ni mtu bora! Mchezaji bora! Alikuwa na sisi miaka 6! Tunamkumbuka!”

No comments:

Powered By Blogger