Friday 15 January 2010

Leo ni Ivory Coast v Ghana!!!!
Huko Uwanja wa Taifa wa Chiazi, Cabinda, Angola, Ivory Coast wakiongozwa na Nahodha wao Supastaa Didier Drogba, leo wanatupa karata yao ya mwisho watakapojimwaga uwanjani kupambana na Ghana, Timu ambayo wengi wameibatiza jina la “Brazil ya Afrika”.
Ivory Coast walitoka suluhu na Burkina Faso 0-0 katika mechi yao ya kwanza na kujitoa kwa Togo kufuatia maafa ya kuuliwa wenzao kumelifanya Kundi hili liwe na Timu tatu tu na hivyo, wakati Ivory Coast wanamaliza mechi zao leo, Ghana ndio kwanza wanaanza.
Ni lazima Ivory Coast ashinde leo ili ajihakikishie ushindi bila ya kungojea kujua matokeo ya mechi ya mwisho kati ya Burkina Faso na Ghana.
Hali hiyo imemfanya Kocha wa Ivory Coast, Vahid Halilhodzic kutoka Bosnia, akiri mambo ni magumu kwao, na amesema: “Tupo pagumu lakini kila kitu kipo mikononi mwetu na tutapigana!”
Nae Dede Ayew, Mtoto wa Nyota wa zamani Ghana, Abedi Ayew Pele, amenena: “Uzuri wa Kundi hili ni kuwa ukishinda mechi moja tu umesonga Raundi inayofuata! Ivory Coast ni timu nzuri na ndio wanapewa nafasi kubwa lakini uwanjani timu zote ni sawa tu!”
Timu ya Ghana imekumbwa na majeruhi kadhaa huku Veterani wao Stephen Appiah yuko nje pamoja na Kiungo Anthony Annan lakini watafarijiki na kuwasili kwa Nyota Michael Essien kujiunga na wenzake baada ya kubaki Klabuni kwake Chelsea kutibiwa misuli iliyokuwa ikimsumbua.
Mechi hii itaanza saa 3 na nusu usiku saa za bongo.
Mechi ya mwisho ya Kundi hili Ghana v Burkina Faso imehamishiwa Mji Mkuu Luanda na itachezwa Uwanja wa Novemba 11 Jumanne ijayo.

No comments:

Powered By Blogger