Waendeshaji wa Ligi Kuu wametamka kuwa watamudu kukabiliana na kutibuliwa kwa Ratiba ya mechi na baridi kali iliyoambatana na barafu nyingi iliyoikumba Uingereza na kusababisha kuahirishwa kwa mechi 7 za Ligi.
Mpaka sasa Ratiba mpya ya mechi zisizochezwa haijatoka na Ligi Kuu imesema inafanya kazi na Vilabu vinavyohusika ili kupanga upya mechi hizo.
Mbali ya mechi hizo 7 za Ligi Kuu kukumbwa na kuahirishwa, pia mechi za Nusu Fainali za Kombe la Carling nazo ziliahirishwa.
Lakini mechi hizo za Carling tayari zimeshapangwa upya na mzunguko wake wa kwanza utachezwa Jumanne na Jumatano ijayo.
Licha ya kutamka kuwa itamudu kupanga Ratiba upya, Ligi Kuu inabanwa na makubaliano yao na FA, UEFA na Wadhamini wa Makombe ya FA na Carling yanayohusu Ratiba ambayo yanawataka kutoa kipaumbele kwa mechi za UEFA CHAMPIONS LEAGUE, EUROPA LIGI na Makombe ya FA na Carling na hivyo kutokupanga mechi za Ligi Kuu siku ambazo mechi za UEFA, FA Cup na Carling Cup zinachezwa.
Ugumu mwingine wa kuipanga upya Ratiba ya Ligi Kuu unakuja kwa vile Msimu huu Ligi Kuu inatakiwa imalizike wiki moja kabla ya kawaida yake ili kuipa nafasi Timu ya Taifa ya England kufanya matayarisho mazuri kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni 11 huko Afrika Kusini.
Kwa hilo, Ligi Kuu haiwezi kuongezwa mbele ya tarehe 9 Mei ambayo inatakiwa kwisha.
Mechi pekee zitakazochezwa na Klabu za England baada ya tarehe 9 Mei ni Fainali ya Kombe la FA hapo Mei 15 na, pengine, Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE hapo Me1 22 endapo Klabu ya England itaingia hiyo Fainali ambayo kwa mara ya kwanza itachezwa Jumamosi badala ya Jumatano tuliyoizoea.
Mkanganyo huu wa Ratiba kupangwa upya umewatia kiwewe baadhi ya Mameneja wa Klabu za Ligi Kuu ambao wanahofia kupangiwa kucheza hadi mechi 5 ndani ya siku 14.
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amesema: “Huwezi kujua. Ratiba inaweza kukupendelea na kukubeba au kuua Msimu wako wote!”
Wasiwasi kama huo pia umeonyeshwa na Arsene Wenger wa Arsenal ambae alitaka mechi zote zilizotakiwa kuchezwa wikiendi ambayo baadhi ya mechi ziliahirishwa zisichezwe ili kuleta usawa kwa Timu zote.
Fergie afurahishwa na Kambi yake Doha
Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson ambae yuko pamoja na Kikosi chake chote Mjini Doha, Qatar kwa ajili ya Kambi ya Mazoezi kwenye Chuo cha Aspire [pichani] amekisifia sana Chuo hicho kwa mapokezi mazuri na pia kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya mazoezi.
Manchester United wapo Doha tangu juzi na watakaa huko kwa siku 4 na hii imekuwa ni nafasi nzuri sana kwao kufanya mazoezi katika hali ya hewa ya joto kidogo ukilinganisha na England ambako sasa ni barafu tu iliyotanda kila sehemu ambayo imefanya mazoezi kwenye Viwanja vya nje kutofanyika.Kikosi hicho cha Man U kitaondoka Doha Alhamisi na Jumamosi kitaingia Uwanjani kwao Old Trafford kucheza na Burnley kwenye Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment