Thursday 14 January 2010

FA CUP: Liverpool kilio!!!
Liverpool imebwagwa nje ya Kombe la FA baada ya kuchapwa 2-1 na Reading hapo jana tena wakiwa nyumbani Anfield na machungu ya kipigo hicho yamezidishwa baada ya Mastaa wao wakubwa wanaowategemea, Steven Gerrard na Fernando Torres, kuumizwa na kulazimika kutoka na hivyo kuleta wasiwasi mkubwa huenda maumivu yao yakawa ya muda mrefu.
Liverpool walipata bao la kuongoxza kibahati pale krosi ya Steven Gerrard ilipoingizwa wavuni na Mchezaji wa Reading Ryan Bertrand.
Reading walisawazisha bao kwa penalti baada ya Liverpool kufanya madhambi ndani ya boksi.
Ndipo mechi ikapelekwa dakika 30 za nyongeza na Reading wakapata bao la pili na la ushindi kupitia Shane Long.
Mechi hii ilikuwa marudiano baada ya Timu hizi kutoka sare huko Reading kwa bao 1-1 na sasa Reading wameingia Raundi ya 4 ya Kombe hili na watacheza na Burnley.
KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA:
Chipolopolo sare na Tai wa Tunisia
Zambia na Tunisia jana zilitoka sare ya 1-1 huko Lubango, Angola katika mechi ya Kundi D.
Zambia walipata bao la kuongoza dakika ya 18 Mfungaji akiwa Jacob Mulenga lakini Tunisia walisawazisha dakika ya 40 kwa bao lilotengenezwa na Youssef Msakni na kufungwa na Souheil Dhaouadi.
Suluhu hii ya Zambia na Tunisia imewafanya Cameroun waliofungwa na Gabon 1-0 hapo jana katika mechi ya awali washike mkia kwenye Kundi hili.
Hapo Jumapili, Januari 17, Zambia wataivaa Cameroun na Tunisia watacheza na Gabon.
Cameroun yazama!!!!
Katika Uwanja wa Taifa wa Tundavala huko Lubango, Angola, Cameroun, moja wa Vigogo wa Afrika, walitolewa nishai na Gabon ambayo licha ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mara 6 haijawahi kushinda hata mechi moja katika Fainali zote hizo.
Goli la Straika wa Hull City ya Ligi Kuu England, Daniel Cousin, la dakika ya 17 ndilo liliimaliza Cameroun.
Baada ya bao hilo, Gabon, wakiongozwa na umahiri wa Kipa wao Ovono walimudu kuyazima mashambulizi yote ya Cameroun yaliyokuwa yakiongozwa na kina Samuel Eto’o, Geremi, Webo, Song na Mastaa wengineo.
VIKOSI:
GABON: Ovono, Ambouronet, Apanga, Moro Mve, Moubamba, Copa, Ndoumbou, Fabrice, Aubameyang, Cousin.
CAMEROUN: Kameni, Song, N’Koulou, Bedimo, Song Billong, Emana, Geremi, Makoun, N’Guemo, Webo, Eto’o.
Mechi zinazofuata za Timu hizi ni Januari 17 Cameroun v Zambia na Gabon v Tunisia.
MECHI ZA Januari 14: [saa za bongo]
[KUNDI D Mjini Luanda]
Mali v Algeria [saa 1 usiku]
Angola v Malawi [saa 3 na nusu usiku]
Burnley yapata Meneja mpya
Brian Laws, miaka 48, ameteuliwa kuwa Meneja mpya wa Klabu iliyomo Ligi Kuu England, Burnley, kuchukua nafasi ya Owen Coyle aliehama wiki iliyokwisha kwenda Bolton Wanderers.
Laws, kabla ya uteuzi huu, alikuwa Meneja wa Sheffield Wednesday lakini alitimuliwa kazi hiyo Mwezi Desemba mwaka jana.
Kibarua cha kwanza cha Laws akiwa Burnley kitakuwa ni mpambano wa huko Old Trafford watakapowavaa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Manchester United siku ya Jumamosi.

No comments:

Powered By Blogger