Sunday 4 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Nyota 5 hazikung’ara!!!
Huko Afrika Kusini kwenye Fainali za Kombe la Dunia, kila mtu alitegemea ndio jukwaa bora kwa Wachezaji Bora duniani kung’ara na kuwika.
Nyota 5 zilizotegemewa kung’ara huko bondeni ni Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney, Kaka na Didier Drogba lakini, baada ya jana Argentina kupokea kipondo cha 4-0 toka kwa Germany, wote hao wamerudi makwao mapema, mikono mitupu na bila kung’ara.
Kati yao Mastaa hao watano, ni wawili tu, Drogba na Ronaldo, ndio walioweza kutingisha nyavu tena ni bao moja moja tu na wote, kwa ujumla, hawakung’ara kabisa na zile cheche zao zilionekana kwa vipindi vifupi tu kama moto uliokuwa unataka kuzimika.
Wadau wamebaki wanakuna vichwa kujiuliza kulikoni?
Lakini, pengine, jibu sahihi limetoka kwa Mtu ambae aliwahi kutamba kuwa ni Bora miongoni mwa Bora wote, Diego Armando Maradona, ambae alihojiwa nini kimewasibu Messi, Rooney na Ronaldo, na akajibu: “Ni gemu tufauti siku hizi. Enzi zetu tulikuwa Wachezaji wachoyo! Mie, nilitaka kufanya kila kitu peke yangu kwenye Timu ndani ya mchezo! Lakini siku hizi, Rooney na Messi, wanajiona kuwa Timu ikiwahitaji ndani ya mchezo ni wajibu wao kucheza kwa ajili ya Timu!”
Inawezekana ni kweli kwani siku hizi ni Mchezo wa Kitimu badala ya Ubinafsi wa Mchezaji!
Mfano hai na sahihi huko Bondeni ni Timu ya Ujerumani isiyokuwa na Supastaa lakini ni hatari mno kama Timu!
Hiyo ndiyo Mashine ya Kijerumani!

No comments:

Powered By Blogger