Sunday 4 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Spain yajikongoja kuingia Nusu Fainali
Spain 1 Paraguay 0
David Villa amefunga bao lake la 5 kwenye Kombe la Dunia huko Afrika Kusini na kuwa ndie aneongoza kwa ufungaji na pia kuiingiza Spain kwenye Nusu Fainali kukutana na Germany.
Villa alifunga bao lake dakika ya 82.
Awali Nelson Valdez wa Paraguay alifunga bao safi lakini lilikataliwa kwa kile kilichodaiwa ni ofsaidi.
Mechi hii ilishuhudia penalti 3 na zote hazikuzaa bao.
Penalti ya kwanza walipewa Paraguay baada ya Refa Carlos Batres toka Guatemala kumwona Gerard Pique akimwangusha Cardozo lakini Cardozo akakosa penalti hiyo baada ya Kipa Casillas kuokoa.
Dakika mbili baadae ikaja zamu ya Spain wakati Alcaraz alipomvaa Villa na Alonso akapiga penalti na kufunga lakini Refa akadai Spain waliingia ndani ya boksi kabla kupigwa na hivyo irudiwe.
Alonso akarudia hiyo penalti na Kipa Villar akaokoa.
Ndipo ikafika dakika ya 82 na likazaliwa goli la ushindi na la kushangaza kwa vituko vyake.
Iniesta alichanja mbuga na angeweza kufunga mwenyewe lakini bila uchoyo akampasia Pedro ambae shuti lake liligonga mwamba na kurudi.
Villa akaunasa mpira huo uliorudi na akaupiga ukagonga posti moja na kwenda kugonga ya pili na kisha kutiririka kuingia wavuni.
Kwa ujumla Spain walicheza mechi hii chini ya kiwango na ikiwa watataka kuifunga Germany mechi ijayo ni lazima wabadilike au Mashine ya Kijerumane itasaga tena Mtu.

No comments:

Powered By Blogger