Sunday, 27 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

England yashindiliwa!!
Germany 4 England 1
England imetupwa nje ya Kombe la Dunia walipotandikwa vibaya na Mahasimu wao wakubwa Germany kwa kushindiliwa bao 4-1 kwenye mechi ya Raundi ya Pili iliyochezwa Free State, Bloemfontein.
Ingawa England ilishindwa vibaya sana lakini mechi hii itakumbukwa kwa Miaka mingi ijayo kwa tukio moja wakati Germany wakiwa mbele kwa bao 2-1 shuti la Frank Lampard kugonga mwamba wa juu, kumpita Kipa Neuer wa Germany na kutua Mita moja ndani ya goli lakini kwa mshangao wa Dunia nzima Refa Jorge Larrionda wa Uruguay ghafla kugeuka kipofu kwa kutokukubali hilo ni goli na kuwaacha Wachezaji wa England wakishika vichwa kwa mfadhaiko na majonzi.
Pengine hiki ni 'kisasi' cha lile goli la Fainali za Kombe la Dunia kati ya England na Germany Mwaka 1966 huko Wembley wakati mechi iko 2-2 Geoff Hurst wa England alipopiga shuti lililogonga posti juu na kudunda chini na kuleta utata kama lilivuka mstari au la lakini Refa kutoka Urusi akasema weka kati na England wakaongeza bao moja na kuwa Mabingwa wa Dunia kwa kuipiga Ujerumani 4-2.   
Mechi hii ilionyesha waziwazi udhaifu mkubwa wa ngome na midifildi ya England kwa jinsi mabao ya Ujerumani yalivyofungwa.
Bao la kwanza la Germany lilianza kwa Kipa Neuer kupiga mpira ndefu wa juu mbele na kumkuta Straika Miroslav Klose akimwacha Beki Matthew Upson na kufunga dakika ya 20.
Mara nyingi goli aina hii unaliona kwa Timu za mchangani.
Mabao mengine matatu ya Germany, lile la Lukas Podolski, dakika ya 32 na mawili ya Thomas Muller, yote ni ya mtindo wa kaunta ataki ulioiacha kiungo na difensi ya England imepotezana na kukatika vibaya.
Germany Robo Fainali atacheza na Mshindi kati ya Argentina na Mexico.
Timu:
GERMANY: Neuer, Lahm, Friedrich, Mertesacker, Boateng, Schweinsteiger, Khedira, Muller, Ozil, Podolski, Klose.
Akiba: Wiese, Jansen, Aogo, Tasci, Kiessling, Badstuber, Trochowski, Cacau, Kroos, Marin, Gomez, Butt.
ENGLAND: James, Johnson, Terry, Upson, Ashley Cole, Milner, Lampard, Barry, Gerrard, Defoe, Rooney.
Akiba: Green, Dawson, Lennon, Crouch, Joe Cole, Warnock, Wright-Phillips, Carragher, Heskey, King, Carrick, Hart.
Refa: Jorge Larrionda (Uruguay)
MECHI ZA JUMATATU Juni 28:
Holland v Slovakia
Holland wataikwaa Slovakia Uwanja wa Moses Mabhida, Durban ili kuwania kuingia Robo Fainali.
Holland mpaka sasa wameshinda mechi zao zote walipozifunga Denmark, Japan na Cameroun kwenye Kundi E.
Wengine ni Argentina pekee ndio imeshinda mechi zote 3 za Kombe la Dunia.
Mshindi kati ya Holland v Slovakia atakutana na Mshindi kati ya Brazil v Chile Robo Fainali Jumamosi ijayo.
Lakini Slovakia, chini ya Kocha Vladimir Weiss, si vibonde baada ya kuwatoa nishai vigogo Italia kwa kuwafunga 3-2 na kuwatupa nje ya Kombe la Dunia.
Holland hawajahi kushinda Kombe la Dunia lakini wamekuwa Washindi wa Pili mara mbili hapo Mwaka 1974 na 1978.
Mwaka 2006 Holland walitolewa Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia na Ureno.
Safari hii, matumaini ya Holland yapo mikononi mwa Mastaa wao Robin van Persie na Arjen Robben ambae amekuwa majeruhi.
Hili ni Kombe la Dunia la kwanza kwa Slovakia na wanawategemea zaidi Wachezaji wao Juraj Kucka, Erik Jendrisek na Miroslav Stoch.
Brazil v Chile
Brazil, Mabingwa wa Dunia mara 5, wanakutana na Chile ambao ni wenzao toka Marekani ya Kusini na Mshindi atacheza na Mshindi wa Holland v Slovakia Robo Fainali.
Brazil bado hawajafungwa kwenye Fainali hizi na wameipiga Korea Kaskazini 2-1, Ivory Coast 3-1 na kutoka sare na Ureno 0-0.
Katika mechi zao za Mchujo huko Marekani ya Kusini ili kupata Timu za kuingia Fainali hizi za Kombe la Dunia, Brazil iliichapa Chile mechi zote mbili kwa bao 3-0 huko Nchini Chile na marudio ni 4-2 huko Brazil.
Lakini huko Afrika Kusini, Chile, chini ya Kocha Marcelo Bielsa, ipo imara na imeshinda mechi mbili kwa kuzifunga Honduras na Uswisi na kupoteza 2-1 na Spain.
Kwenye mechi hii, Marco Estrada wa Chile hatacheza baada ya kupewa Kadi Nyekundu kwenye mechi na Spain.
Brazil watamkaribisha tena Supastaa Kaka aliefungiwa mechi ya mwisho na Ureno baada ya kupewa Kadi Nyekundu ya uonevu Brazil walipocheza na Ivory Coast.
Pia Mchezaji wa zamani wa Manchester City, Elano, alieumizwa kwenye mechi ya Brazil v Ivory Coast amepona na atarudi Uwanjani kuimarisha Kiungo cha Brazil.

No comments:

Powered By Blogger