Monday 28 June 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Holland kuivaa Brazil au Chile Robo Fainali
Holland leo wameifunga Slovakia bao 2-1 na Robo Fainali watacheza na Mshindi kati ya Brazil au Chile wanaocheza baadae leo.
Walikuwa ni Arjen Robben na Wesley Sneijder waliofunga mabao ya Holland na kuendeleza libeneke la Timu hiyo maarufu kwa jina la 'Chungwa' kufuatana na rangi zao.
Slovakia walipata bao lao dakika ya 90 kwa penalti iliyofungwa na Vittek baada ya Kipa wa Uholanzi Sketelenburg kumwangusha Jakubko.
Sketelenburg alitwangwa Kadi ya Njano kwa tukio hilo.
TATHMINI MECHI ZA Jumanne Juni 29
Spain v Portugal
Hii ni mechi yenye mvuto kwa wengi na ina ushindani wa jadi kwani Nchi hizi ni majirani.
Spain ndio Mabingwa wa Ulaya lakini kwenye Kombe la Dunia Miaka ya hivi karibuni Ureno ndio wenye rekodi nzuri walipomaliza nafasi ya 4 Mwaka 2006 huku Spain ikitolewa Raundi ya Pili tu.
Kwenye Kundi H, Spain walianza vibaya walipofungwa na Uswisi lakini wakaibuka na kuzitandika Honduras na Chile mechi zilizofuata na kuwa vinara wa Kundi hilo.
Ureno walimaliza wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Brazil toka Kundi G wakitoka sare 0-0 na Brazil na Ivory Coast lakini waliinyuka Korea Kaskazini 7-0.
Ureno chini ya Carlos Queiroz ndio Timu pekee kwenye Fainali hizi za Kombe la Dunia bado haijafungwa hata goli moja.
Wakati Mastaa wa Timu zote mbili, Fernando Torres na Cristiano Ronaldo, hawajaonyesha cheche zozote huku Torres akiwa hana hata bao moja baada ya mechi 3, wamebaki Wachezaji wengine kama David Villa wa Spain, ndio wanabeba Timu zao.
Timu zote huenda zikawakosa Wachezaji muhimu kwa Spain kumkosa Alonso na Ureno kumpoteza Danny kwa kuwa na maumivu.
Paraguay v Japan
Japan wanaingia mechi hii kwa kuzifunga Timu ngumu Denmark na Cameroun toka Kundi lao na hivyo ndio wanaoonekana kama ni bora lakini Paraguay wanacheza staili tofauti ya kutumia nguvu na kucheza kitimu na mpaka sasa wamefungwa bao moja tu kwenye mechi ya sare ya 1-1 na waliokuwa Mabingwa wa Dunia Italia.
Chini ya Kocha Gerardo Martino na jopo la Wachezaji mahiri kama Roque Santa Cruz, Lucas Barrios, Nelson Valdez na Oscar Cardozo, Paraguay si mzaha.
Nao Japan, chini ya Kocha Takeshi Okada, wana Timu inayojituma kwa nguvu kazi ya pamoja ya Wachezaji kama Keisuke Honda, Yasuhito Endo na ‘Mbrazil’ Tulio Tanaka.
Hii ni mechi ngumu kuitabiri.

No comments:

Powered By Blogger