Friday 2 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

Ghana ni kitimtim!!
Jana Julai 1, Nchini Ghana ilikuwa ni mapumziko kusheherekea Siku yao ya Jamhuri lakini sherehe hizo huenda zikaendelea leo Nchini humo, na pengine Afrika yote, endapo Ghana wataifunga Uruguay na kutinga Nusu Fainali za Kombe la Dunia.
Wakipata mafanikio hayo, Ghana itakuwa Nchi ya kwanza kutoka Afrika kufika hatua hiyo.
Mechi hiyo inachezwa Uwanja wa Soccer City, Soweto, Jijini Johannesburg, Afrka Kusini lakini Ghana nzima inazizima kwa matarajio huku viroho vikidunda.
Jijini Accra, Mji Mkuu wa Ghana, Bigi Skrini zimeendelea kuwekwa sehemu mbalimbali ili Wananchi waweze kuona pambano hilo laivu.
Kwa sasa, zinafanywa ibada maalum ili kuiombea heri ‘Nyota Nyeusi’ kama Timu ya Ghana inavyojulikana.
Port Elizabeth yabanana!!
Uwanja wa Nelson Mandela, Port Elizabeth, Afrika Kusini umeshatumika kwa mechi 5 za Kombe la Dunia mpaka sasa na hakuna hata mechi moja kati ya hizo uliojaza Uwanja huo wenye kuchukua Watu 42,00 lakini leo wakati Brazil inacheza na Holland, hali ni tofauti kwani hamna hata upenyo wa kukaa.
Mbali ya Uwanja, katika kila Hoteli na Nyumba za Kupanga, utakutana na bango: ‘Vyumba Vimejaa.’
Benayoun njiani Stamford Bridge
Chelsea wanakaribia kumchota Kiungo wa Liverpool Yossi Benayoun kwa Mkataba wa Miaka minne na dau la Pauni Milioni 5.5.
Benayoun, Miaka 30, alijiunga na Liverpool Mwaka 2007 akitokea West Ham na ameichezea Liverpool mechi 91 na kufunga bao 18.
FIFA yaipa Nigeria Masaa 24
FIFA imeitaka Nigeria ifute uamuzi wake wa kujitoa kushiriki Mashindano ya Kimataifa kwa Miaka miwili la sivyo watasimamishwa uanachama FIFA.
Habari hizi zimethibitishwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke.
Uamuzi wa kuitoa Nigeria kwenye Mashindano ya Kimataifa kwa Miaka miwili ulichukuliwa na Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan baada ya Timu hiyo kutolewa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Dunia kwa kushika mkia kwenye Kundi lao.
Valcke ametamka: “Huwezi kuruhusu Serikali ziingilie Soka! Ufaransa tuliionya sasa kwa nini tushindwe kwa Nigeria? Tuna Wanachama 208 na tukiruhusu mmoja aanze kukiuka kanuni za Soka, mhimili wote wa Soka utaporomoka!”
Makocha Timu zilizotolewa Kombe la Dunia wazidi kutimka!!
Kocha wa Japan, Takeshi Okada, amejitoa toka Timu ya Japan baada ya Nchi hiyo kutolewa nje ya Kombe la Dunia na Paraguay kwenye mechi ya Raundi ya Pili ilipofungwa kwa penalti 5-3 baada ya mechi kuwa sare 0-0 kwa dakika 120.
Okada sasa amejiunga kwenye listi ya Makocha waliobwaga manyanga kufuatia kubwagwa nje ya Kombe la Dunia ambayo wapo Kocha wa Ugiriki, Otto Rehhagel, Javier Aguirre wa Mexico na Huh Jung-moo wa Korea ya Kusini.
Bila shaka, listi hii itaongezeka.

No comments:

Powered By Blogger