Thursday, 1 July 2010

CHEKI: www.sokainbongo.com

KOMBE LA DUNIA:
ROBO FAINALI: Tathmini
Holland v Brazil
Uwanja: Nelson Mandela Bay, Port Elizabeth
Saa: 11 jioni [bongo]
Timu hizi zimekutana mara 3 tu kwenye Kombe la Dunia na mechi zote hizo zilikuwa ni ‘Vita Takatifu’.
Mwaka 1974, huko Ujerumani, Holland iliifunga Brazil 2-0 kwenye Kundi lao na walifika Fainali ya Kombe la Dunia na kufungwa 2-1 na Ujerumani waliotwaa Ubingwa wa Dunia.
Mwaka 1994 huko USA, katika mechi ya Robo Fainali, Brazil waliinyuka Holland 3-2 na wakaendelea hadi Fainali na kuitoa Italia na kuwa Mabingwa wa Dunia.
Huko Ufaransa, Mwaka 1998, Brazil na Holland zilikutana Nusu Fainali na Brazil wakaibwaga Holland kwa matuta na kuingia Fainali waliyotolewa na Ufaransa.
Mpaka sasa Timu zote hazijaonyesha ile desturi yao, kwa Brazil kucheza Samba, yaani ‘Soka Tamu’, na Holland kucheza ule mpira uitwao ‘Soka Kamili’ ingawa kila Timu ni tishio kubwa.
Brazil itamkosa Ramires ambae amefungiwa mechi moja baada ya kuzikwaa jumla ya Kadi za Njano mbili na hivyo huenda wakamchezesha Dani Alves badala yake.
Pia Brazil watamkosa Kiungo Elano ambae ameumia enka.
Holland hawana wasiwasi wa kukosa Wachezaji na hata Staa wao Arjen Robben aliekuwa akisuasua kwa kuwa majeruhi sasa yuko fiti.
Makocha:
Dunga wa Brazil anataka kuifikia rekodi aliyoweka Franz Beckenbauer wa Ujerumani ya kunyakua Kombe la Dunia akiwa Mchezaji na pia Kocha.
Nae Kocha wa Uholanzi Bert Van Marwijk ni mzoefu, anaepanga vizuri mambo na ni mtulivu.
Sifa hizo ndizo bora kwa Uholanzi ambayo kihistoria hukumbwa na migogoro kwenye kila Timu zao hasa wakati wa Mashindano makubwa.
Mbinu:
Kila Kocha hupenda kutumia Viungo wawili wanaocheza Difensi, mbele ya Mabeki wanne, na kuachia Washambuliaji wanne wahangaike huku wakiongozwa na Mchezaji mmoja ambae ndie mchezeshaji.
Mchezeshaji kwa Brazil ni Kaka na Uholanzi ni Wesley Sneijder.
Nini wanasema:
Bert Van Marwijk: “Sisi ni Taifa dogo lakini ni wabunifu na kama anavyosema Johan Cruyff [Staa wa zamani Uholanzi] tuna ‘kiburi’ fulani kwenye Soka! Tutatumia kiburi hicho kitupe mafanikio!”
Dunga: “Holland wana staili ya uchezaji kama yetu. Wao ni kama Timu ya Marekani ya Kusini.”
Vikosi:
Holland (Fomesheni: 4-2-3-1): Stekelenburg; Van der Wiel, Heitinga, Mathijsen, Van Bronckhorst; Van Bommel, De Jong; Robben, Sneijder, Kuyt; Van Persie.
Brazil (Fomesheni: 4-2-3-1): Julio Cesar; Maicon, Lucio, Juan, Michel Bastos; Gilberto Silva, Melo; Dani Alves, Kaka, Robinho; Luis Fabiano
Refa: Yuichi Nishimura (Japan).
Uruguay v Ghana
Uwanja: Soccer City, Soweto, Johannesburg
Saa: 3.30 [bongo]
Uruguay ni Mabingwa wa Dunia mara mbili kwa kulichukua Kombe la Dunia Mwaka 1930 na 1950.
Ghana ni Nchi ya 3 toka Afrika kufikia hatua ya Robo Fainali nyingine zikiwa ni Cameroun Mwaka 1990 na Senegal 2002.
Lakini safari hii, kwa mara ya kwanza, Kombe linachezewa Afrika na Afrika yote inaomba Ghana ifanikiwe.
Uruguay wamefika hatua hii baada ya kutofungwa kwenye Kundi lao walipotoka sare na Ufaransa na kuzifunga Afrika Kusini na Mexico.
Raundi ya Pili wakaipiga Korea Kusini 2-1.
Ghana wamefika hapa walipoishinda Serbia 1-0, kutoka sare na Australia ya 1-1 na kufungwa na Germany 1-0.
Raundi ya Pili, Ghana wakaitupa nje USA 2-1 baada ya dakika 120 za Soka.
Uruguay itamkosa Diego Godin ambae ana maumivu lakini wengine wote wako fiti na mashambulizi yao yanategemewa kuongozwa na Diego Forlan, Suarez na Cavani.
Ghana walikuwa na wasiwasi na Asamoah Gyan alieumia pamoja Kevin-Prince Boateng lakini wote wanategemewa kuwa fiti.
Nae Kiungo wa Inter Milan Sulley Muntari anategemewa kuanza kwa vile Dede Ayew, Mwana wa Abedi Pele, amefungiwa mechi moja baada kupata Kadi za Njano mbili.
Ghana pia itamkosa Jonathan Mensah ambae amefungiwa kama Ayew.

No comments:

Powered By Blogger