Thursday 12 November 2009

Chelsea yapata pigo, Bosingwa nje miezi mitatu!!
Fulbeki wa kulia wa Chelsea Jose Bosingwa atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu baada ya kupasuliwa goti la kushoto ambalo aliumia katikati ya mwezi Oktoba.
Bosingwa, miaka 27, alijiunga Chelsea Mei 2008 kutoka Klabu ya Nchini kwao Ureno FC Porto.
Chelsea vilevile wana pengo kwa Fulbeki wao wa kushoto Ashley Cole ambae alipata ufa kwenye mfupa wa ugoko mguuni lakini habari njema kwao ni kuwa hahitaji upasuaji ingawa atakuwa nje mwezi mzima.
Ingawa Chelsea imepata afueni baada ya CAS, Mahakama ya Usuluhishi kwenye Michezo, kuisimamisha adhabu waliyopewa na FIFA ya kutosajili Mchezaji hadi 2011 baada ya kuvunja sheria walipomteka Chipukizi Gael Kakuta kutoka Lens ya Ufaransa, Klabu hiyo imesema haisajili mtu dirisha la usajili litakapokuwa wazi Januari 2010 licha ya ukweli watakuwa na pengo kuu mwezi huo wa Januari wakati Wachezaji wao akina Didier Drogba, Salomon Kalou, Michael Essien na John Obi Mikel watakapokuwa Angola kuchezea Nchi zao Kombe la Mataifa ya Afrika.
Fergie awatakia heri Wachezaji wake waliomo kimbembe cha Kombe la Dunia wikiendi hii!!
Wachezaji wanne wa Manchester United wako kwenye vita kubwa Jumamosi hii na Jumatano ijayo ili kuzifanikisha Nchi zao kuingia Fainali za Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini kwa karata ya mechi za mchujo na wote wametakiwa kila la heri na Meneja wao Sir Alex Ferguson.
Wachezaji hao wanne ni Patrice Evra, Nani, John O'Shea na Darron Gibson.
Wachezaji O’Shea na Gibson watachezea Nchi yao Republic of Ireland na watapambana na Patrice Evra na Ufaransa yake.
Ferguson amenena: “Ireland inabidi washinde mechi ya kwanza kwao uwanjani Croke Park, Ireland ili wawe na nafasi kwani ni ngumu kwao kushinda ugenini Paris!”
Kuhusu Mchezaji wake mwingine Nani na Ureno ambayo Kocha wao ni Msaidizi wake wa zamani Carlos Queiroz wanaocheza na Bosnia-Herzegovina , Ferguson ametamka: “Ni mechi ngumu! Bosnia walimaliza Kundi lao nyuma ya Spain, sio watu rahisi! Mechi ambayo Ureno watajutia ni ile na Denmark wakiwa nyumbani wanaongoza 2-1 na bado dakika 5 tu lakini wakafungwa 3-2, hilo liliwafanya wakose kuongoza Kundi lao! Angekuwa Ronaldo fiti ningesema wana uhakika kuwafunga Bosnia lakini bila ya yeye ni ngumu! Ila naomba kwa ajili ya Carlos Queiroz washinde!”

No comments:

Powered By Blogger